Alhamisi , 30th Jun , 2016

Waziri wa nchi ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, (TAMISEMI), Mhe. George Simbachawene amewataka wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya wapya kuwa kiunganishi kati ya serikali na wananchi ili kumaliza matatizo yiliyopo katika jamii.

Waziri wa nchi ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, (TAMISEMI), Mhe. George Simbachawene.

Waziri Simbachawene, ametoa kauli hiyo katika semina ya maadili ya viongozi hao iliyofanyika jijini Dar es Salaam, amesema kuwa wananchi wanahitaji huduma ya viongozi hao wakati wote bila kujali itikadi zao.

Aidha Waziri Simbachawene amewataka viongozi hao kushirikiana na taasisi mbalimbali katika maeneo yao ikiwemo taasisi mbalimbali za kidini, taasisi binafsi pamoja na taasisi za umma.

Pia Waziri Simbachawene amewataka viongozi hao kutokuwa chanzo cha migogoro katika maeneo yao na wasimamie sheria za nchi katika kuwaongoza wananchi wanaowaongoza.