Jumatatu , 10th Jul , 2023

Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) iliyokutana chini ya Mwenyekiti wake Rais Samia Suluhu Hassan, ilipokea na kujadili kwa kina taarifa ya makubaliano ya uwekezaji na uendeshaji wa bandari na kuazimia kwamba serikali ihakikishe maoni chanya na yenye tija kutoka kwa wananchi yanasikilizwa.

Rais Samia alipoongoza kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC)

Taarifa hiyo imetolewa leo Julai 10, 2023, na Katibu wa Itikadi na uenezi wa CCM Sophia Mjema, na kuongeza kuwa serikali iongeze kasi ya kutoa elimu kwa wananchi juu ya uhalisia uliomo katika makubaliano ya uwekezaji na uendeshaji huo wa bandari.

Kikao hicho cha NEC, kilitanguliwa na kikao cha Kamati Kuu (CC) ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa iliyoketi mapema, asubuhi ya tarehe 9, Julai 2023.

Aidha, Halmashauri Kuu ya CCM Taifa iliazimia kuwa uwekezaji na uendeshaji wa bandari ni kwa manufaa ya uchumi wa nchi na kwamba uwekezaji huo ni utekelezaji wa vitendo wa Ilani ya CCM ya Mwaka 2020- 2025, ibara ya 59, ukurasa wa 92.