Jumatatu , 4th Aug , 2014

Asasi ya utetezi wa upatikanaji wa huduma bora za afya nchini Tanzania ya SIKIKA, imeelezea kusikitishwa kwa namna uongozi wa halmashauri ya wilaya ya Kondoa ulivyopiga marufuku asasi hiyo kufanya shughuli zake katika halmashauri hiyo.

Waziri wa nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Bi. Hawa Ghasia.

SIKIKA imezuiliwa kufanya shughuli zake kwa madai ya kutoa kauli ya dharau kuwa madiwani katika halmashauri ya wilaya ya Kondoa hawajui kusoma, madai ambayo hata hivyo yamekanushwa vikali na uongozi wa bodi ya SIKIKA.

Mkurugenzi mkuu wa SIKIKA Irenei Kiria amesema hayo leo jijini Dar es Salaam huku akiitaka wizara ya serikali za mitaa na tawala za mikoa kuchunguza kitendo cha wao kuzuiliwa kufanya shughuli zake huku akimtaka mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali kufanya ukaguzi maalumu wa idara ya afya katika halmashauri hiyo.

Wakati huohuo, Baraza la watu waishio na virusi vya ukimwi wilaya ya Arusha, KONGA, limekabidhi msaada wa fedha taslimu shilingi milioni 3, kwa vikundi 10 vya watu wanaoishi na virusi vya ukimwi katika wilaya hiyo, ili kuwainua katika biashara zao.

Akiongea jijini Arusha, Mwenyekiti wa KONGA wilaya ya Arusha, Jane Mwiliego wakati akikabidhi fedha hizo, kwa vikundi 10 vyenye idadi ya watu 150, amesema fedha hizo zimetolewa na halmashauri ya Jiji la Arusha kwa ajili ya kusaidia baraza hilo, ambalo linakabiliwa na changamoto mbalimbali.

Alisema wamefikia hatua ya kutoa fedha hizo baada ya kutembelea vikundi hivyo na kubaini kuwa vinakabiliwa na upungufu mkubwa wa mitaji, kwa ajili ya kuendeleza biashara zao ili kujikwamua kiuchumi ili kuviwezesha vikundi hivyo vya watu waishio na virusi vya UKIMWI, ambavyo vimekosa mwelekeo.