Alhamisi , 1st Jan , 2015

Waziri mkuu Mizengo Pinda amesema bado ana dhamira ya dhati ya kumsaidia rais Jakaya Kikwete katika uongozi wa taifa la Tanzania na kuongeza kasi ya kuwahudumia wananchi, ili waweze kujiletea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Waziri mkuu Mizengo Pinda

Waziri Mkuu ameyasema hayo wilayani mpanda mkoani Katavi kwenye sherehe za mkesha wa kuuaga mwaka 2014 na kuupokea mwaka mpya wa 2015.

Amesema baada ya kumalizika kwa sakata la akaunti ya Tegeta Escrow lililokuwa linawatuhumu viongozi mbalimbali, amesema yeye alikuwa na imani kwamba tuhuma hizo zisingemgusa kwa sababu katika uongozi wake amekuwa akizingatia misingi ya uadilifu na utawala bora.

Ameongeza kuwa, yeye binafsi amekuwa akipiga vita vitendo vya rushwa na kamwe hajawahi kupokea wala kutoa rushwa.
 
Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Katavi Dk Ibrahimu Msengi akiongea wakati wa sherehe hizo za kuupokea mwaka mpya, amesema mkoa wa Katavi umepiga hatua kubwa kimaendeleo baada ya kutekeleza maagizo mengi ya serikali ikiwemo kuhimiza masuala ya kilimo, ufugaji, uvuvi, elimu na ujenzi wa nyumba bora kama njia kuu za wananchi kujiletea maendeleo.