Alhamisi , 10th Dec , 2015

Rais Mstaafu wa awamu ya Nne Dkt. Jakaya Kikwete jana ameungana na wakazi wa mji wa Chalinze kufanya usafi huku akiwataka watanzania wamuunge mkono Rais Dkt. Magufuli kupambana na wafanyabiashara na watu wengine wanaokwepa kulipa kodi.

Rais Mstaafu Dkt Jakaya Mrisho Kikwete na mkewe Mama Salma Kikwete wakifanya usafi katika soko kuu la Chalinze Desemba 9, 2015

Akizungumza na wakazi wa eneo hilo Dkt. Kikwete amesema kazi aliyoianza Dkt. Magufuli ya kupambana na wakwepa kodi ni nzuri na ni mfano wa kuigwa kwani itasaidia kuimarisha uchumi.

Aidha Rais huyo mstaafu ameeleza masikitiko yake juu ya wanaomtuhumu kuwa enzi za utawala wake alishindwa kusimamia ukwepaji ulipaji kodi na kutoka misamaha isiyokuwa na tija kwa serikali.

Dkt. Kikwete ameongeza kuwa wanaomshambulia wanaonekana ni jinsi gani wamefirisika kisiasa, na kusema kuwa yote wanayoyafanya ni siasa za maji taka na kuwataka waendelee ila wamuache Rais magufuli afanye kazi yake.

Rais mstaafu Kikwete amesema hajawahi kushiriki na mfanyabiashara yoyote katika ukwepaji kodi na kuongeza kuwa endapo angefanya hivyo kwa miaka 10 deni hilo lisingefika milioni 900.