Jumatatu , 26th Aug , 2024

Sheria ya haki ya kuzima simu imeanza kutumika nchini Australia, ikitoa unafuu kwa watu ambao wanahisi kulazimishwa kupiga simu au kusoma ujumbe kutoka kwa waajiri baada ya kumaliza kazi yao ya siku.

Sheria hiyo mpya inaruhusu wafanyakazi kupuuza mawasiliano ya mabosi wao baada ya saa kadhaa iwapo watachagua, bila hofu ya kuadhibiwa na mabosi zao.

Utafiti uliochapishwa mwaka jana ulikadiria kuwa Waaustralia walifanya kazi kwa wastani wa masaa 281 ya muda wa ziada usiolipwa kila mwaka.Zaidi ya nchi 20, hasa katika bara la  Ulaya na Amerika ya Kusini zina sheria sawa.

Sheria hiyo haikatazi waajiri kuwasiliana na wafanyakazi baada ya saa kadhaa badala yake, inawapa wafanyakazi haki ya kutojibu isipokuwa kukataa kwao kunachukuliwa kuwa sio busara. 

Chini ya sheria, waajiri na wafanyakazi wanapaswa kujaribu kutatua migogoro kati yao. Ikiwa hiyo haitafanikiwa kupata azimio Tume ya Kazi ya Haki ya Australia (FWC) inaweza kuingia.