Jumatano , 2nd Jul , 2014

Shekh mkuu wa Tanzania, Mufti Issa Bin Shaaban Simba, ametoa tamko juu ya mgogoro wa muda mrefu wa uongozi unaukabili msikiti mkuu wa Ijumaa wa mkoa wa Arusha

Shekh mkuu wa Tanzania, Mufti Issa Bin Shaaban Simba, ametoa tamko juu ya mgogoro wa muda mrefu wa uongozi unaukabili msikiti mkuu wa Ijumaa wa mkoa wa Arusha na msikiti mdogo wa masjid Quba ambalo limeweka bayana viongozi wanaostahili kuiongoza misikiti hiyo kwa mujibu wa sheria

Akitoa tamko hilo mbele ya baadhi ya waumini na viongozi wa kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa wa Arusha Shekh mkuu amesema viongozi wapya waliopewa jukumu la kuongoza misikiti hiyo ambao waliondolewa na kikundi cha waumini, wako kwa mujibu wa sheria na ndio wanaotambulika na wala sio vinginevyo

Hata hivyo baada ya shekh mkuu kutoa tamko hilo viongozi walioondolewa madarakani wamesema hawatambui tamko la shekh mkuu Muft Issa Shaaban Simba kwani limetolewa wakati tayari kesi iko mahakamani.

Kwa mujibu wa tamko la sheikh Simba, msikiti mkuu wa Ijumaa utaongozwa na Sheikh wa mkoa Shaban bin Jumaa Abdallah, na kaimu katibu wa mkoa, ustadhi Abdallah Masoud na mwenyekiti wa halmashauri ustadhi Mohamed Juma Marawi.
Na msikiti wa masijid Quba utaongozwa na Sheikh Hassan Waziri ambaye ni imamu na Abubakar Sharif, mweka hazina Chohan Jumbe.

Mgogoro huo wa muda mrefu sasa licha ya kusababisha mgawanyiko wa waislam na ukosefu wa amani katika misikiti hiyo umesababisha miradi ya waumini wa dini hiyo iliyoko katika maeneo hayo kufungwa ikiwemo shule ya sekondari ya Bondeni