Waziri wa Nishati Kalemani
Akiwa ziarani wilayani Muheza mkoani Tanga, Naibu Waziri wa Nishati, Bi Subira Mgalu amesema kwamba Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kutekeleza jukumu hilo pasipo kukatishwa tamaa na kusisitiza kuwa wamedhamiria kuwafikishia huduma ya umeme watanzania wote bila kubagua aina ya makazi yao.
Amesema Wataalamu wa serikali wamekuwa wakihakikisha taratibu za usalama zinafuatwa wakati wa kuunganisha umeme katika nyumba za vijijini, hususani zilizoezekwa kwa makuti au nyasi
"Kumekuwepo na maneno ya baadhi ya watu kubeza jitihada zinazofanywa na Serikali kuwaunganishia umeme watanzania wote hususani waishio vijijini pasipo ubaguzi, wakitoa sababu kwamba wenye nyumba za nyasi hawastahili kupatiwa huduma hiyo", amesema Mhe. Subira Mgalu.

Naibu Waziri Subira Mgalu akiwa ziarani Muheza.
Ameongeza, "niwatake wananchi kuondoa hofu, kuwa madhara yanaweza kutokea katika nyumba za nyasi ambazo zimeunganishiwa umeme na badala yake muwapuuze watu wanaobeza jitihada hizo, na zaidi muutumie umeme kujiletea manufaa katika maisha yenu".
Amefafanua kwamba kazi ya kuwapelekea wananchi wa vijijini umeme inafanyika sambamba na zoezi la uhamasishaji wa kujenga makazi bora, na kwamba mwananchi mwenye makazi duni akiunganishiwa umeme, anapata hamasa ya kuboresha zaidi makazi yake.
Pamoja na hayo amesisitiza kwamba maelekezo kwa wakandarasi ni kutobagua nyumba ya aina yoyote na kwamba Watanzania wote wanahitaji umeme pasipo ubaguzi wa aina ya makazi.



