Jenista Mhagama, Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu.
Wito huo umetolewa leo na Waziri wa nchi ofisi ya waziri Mkuu Sera, Uratibu wa bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu, Jenista Mhagama wakati akizungumza na wanachama wa chama cha wafanyakazi nchini wa viwandani, biashara, taasisi za fedha, huduma na ushauri (TUICO) kwenye mkutano mkuu wa tano wa chama hicho mjini Dodoma.
Mhagama amesema kuwa kuna baadhi ya waajiri nchini ambao hawataki wafanyakazi wao kujiunga na vyama vya wafanyakazi nchini kitendo alichosema ni ukiukwaji wa sheria za nchi.
Aidha amemwagiza katibu mkuu wa shirikisho la vyama vya wafanyakazi nchini (Tucta), Nicolaus Mgaya kufuatilia utendaji kazi wa viongozi wa vyama vya wafanyakazi mahali pa kazi na endapo utendaji wao wa kazi utakuwa hauridhishi waondolewe baada ya utaratibu wa kisheria kufuatwa.
Amesema hiyo inatokana na baadhi yao kuwa vyanzo vya migogoro baina ya wafanyakazi na waajiri kutokana na viongozi hao kuacha kutekeleza majukumu yao ya kuwatetea wafanyakazi na badala yake wanaungana na waajiri kuwakandamiza wafanyakazi wenzao.
Naye Jaji mfawidhi wa mahakama kuu nchini, Aisha Nyerere amewataka viongozi wa vyama vya wafanyakazi nchini kuwatumikia wafanyakazi ili kuondokana na dhana iliyojengeka kwa baadhi ya wafanyakazi kuwa wanafanyakazi kulingana na matakwa ya waajiri.
Kwa upande wake katibu mkuu wa Tucta, Nicolaus Mgaya amewataka viongozi wa vyama vya wafanyakazi kutetea maslahi ya wafanyakazi kwani pamoja na majukumu mengine waliyonayo ni jukumu lao la msingi kutetea maslahi ya wafanyakazi wanaowatumikia.