Jumatatu , 1st Feb , 2016

Serikali yavunja mkataba ulioingia na mwekezaji katika kiwanda cha kuchakata chai cha Mponde kilichopo Bumbuli Wilayani Lushoto Mkoani Tanga baada ya mwekezaji huyo kushindwa kukiendesha na kukisababishia madeni ya zaidi ya shilingi bilioni 3.

Msajili wa hazina kutoka ofisi ya msajili wa hazina Laurence Mafuru,

Awali akitangaza kuvunjwa kwa mkataba huo rasmi msajili wa hazina kutoka ofisi ya msajili wa hazina Laurence Mafuru amesema wamevunja rasmi mkataba huo kutokana na kukiukwa kwa makubaliano waliyowekeana na mwekezaji huyo kushindwa kuyatekeleza ipasavyo.

Aidha amesema kwa muda wa miaka mitatu sasa kiwanda hicho kilisimama kufanya shughuli za uzalishaji kutokana na mgogoro uliokuwepo baina ya wakulima na mwekezaji huyo hali iliyopelekea wakulima wa zao hilo kuyumba kimaisha.

Mafuru amesema lengo la serikali ni kuhakikisha inafufua na kuviendeleza viwanda vilivyopo Nchini kwa maslahi ya wananchi wake ikiwa ni pamoja na kukuza pato la mtu mmoja mmoja sambamba na kuinua uchumi wa eneo husika.

Amesema serikali ilifuata taratibu na sheria ya kusitisha mkataba huo hivyo wametengeneza menejimenti ya muda mfupi itakayoendesha na kuboresha kiwanda hicho chini ya usimamizi wa bodi ya chai ili kianze kazi ya uchakataji chai kwa haraka.