Waziri wa Katiba na Sheria nchini Tanzania, Dkt. Asha-rose Migiro.
Akizungumza Bungeni jana Mjini Dodoma Waziri wa Katiba na Sheria nchini Mh, Dkt. Asha-rose Migiro amesema Serikali haitavumilia upotoshaji wa wanasiasa na kuwataka wananchi wasishawishiwe kufanya vurugu na kuandamana na kusema pindipo atakaefanya hivyo basi Sheria itakuachukua mkondo wake.
Dkt, Migiro amesema kuwa Mahakama imeridhia kuendelea na mchakato huo kama ulivyopangwa na kuwataka wananchi wasubiri Katiba itakayopendekezwa na kuongeza kuwa Vyama vya siasa vitakaa tena chini ya kituo cha Demokrasia Tanzania ili kupata maridhiano juu ya katiba hiyo.
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba Samwel Sitta ametangaza kuwa zoezi la kuipigia kura rasimu ya Katiba litafanyika kuanzia tarehe 29 mwezi huu hadi Oktoba 2 ama 3 ili kupata Katiba iliyopendekezwa.
Akihairisha kikao cha Bunge hilo jana usiku Sitta amesema kabla ya zoezi hilo la kupiga kura itafanyika kazi ya wajumbe kupitia na kuidhinisha Ibara zote karibu 300 kwa utaratibu utakaopangwa.
Amesema kwa hali ilivyo itachukua siku 300 kupitia na kuridhia Ibara zote kwa kumhoji mjumbe mmoja mmoja kwa wajumbe wote 460 wakati wamepewa siku 60 tu hivyo kamati ya uongozi itabidi ije na utaratibu utakaokoa muda.