Mafundi na wafanyakazi wa eneo la Magereji Tegeta
Akizungumza na wananchi wa eneo la Tegeta Magereji katika Manispaa ya Kinondoni, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mh. Paul Makonda amesema uamuzi huo wa kuzirejesha hekari hizo umekuja kufuatia vikao kadhaa vya majadiliano baina ya mwekezaji na serikali ili kumuomba aligawe sehemu ya eneo hilo kufuatia jitihada za awali za kulirejesha eneo hilo kupitia mahakama kugonga mwamba .
Makonda ameongeza kuwa mara baada ya kumuomba na kumsihi muwekezaji huyo alikubali kuzitoa hekari hizo na kuzikabidhi kwa wananchi hao ambao wamekuwa wakiishi na kulitumia eneo hilo kwa kipindi kirefu .
Aidha Makonda amewataka wananchi hao kusubiri hati ya eneo hilo ambayo inataraji kutoka ndani ya wiki mbili kwa ajili ya matumizi mengine ikiwemo kuombea mikopo na shughuli nyingine kama ambavyo wamemuomba kuweza kumlipa muwekezaji huyo eneo lililosalia la hekari 14 ili waweze kulitumia kwa ajili ya shughuli zao za kiufundi na makazi

Paul Makonda - Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam
Pia amewaahidi wananchi hao kuweza kuwakabidhi shughuli zote za ufundi wa magari za jiji la Dar es Salaam ili ziweze kuendeshwa chini yao.
Kwa upande wa mwakilishi wa mafundi hao takriban elfu 10, MUNIR RAMADHAN amesema wanaishukuru serikali kwa jitihada za kuwarejeshea sehemu ya eneo la ardhi lakini wakibainisha kuwa wapo tayari kulinunua eneo lililo salia la hekari 14 ili wasipate adha ya kuhamisha mali na watu waliokuwepo hapo .



