Alhamisi , 22nd Jan , 2015

Wananchi wa kijiji cha Namba Tisa wilayani Kahama mkoani Shinyanga wamepigwa marufuku kutumia maji yanayoririkia kutoka mgodi wa dhahabu wa bulyanhulu yanayosadikiwa kuwa na sumu.

Serikali imepiga marufuku wananchi wa kijiji cha Namba Tisa kata ya Bulyanhulu wilayani Kahama mkoani Shinyanga kilichokaribu na mgodi wa dhahabu wa bulyanhulu  unaomilikiwa na kampuni ya Acacia kutumia maji ya visima pamoja na kuendesha shughuli za kilimo katika eneo hilo kufuatia kuvuja kwa bwawa la maji ya yanayodhaniwa  kuwa na sumu ya cyanide.
 
Akitoa agizo hilo la serikali mbele ya waandishi wa habari  mkuu wa wilaya ya Kahama, Benson Mpesya amesema serikali imeamua kupiga marufuku utumiaji wa maji ya visima pamoja na kuendesha shughuli za kilimo katika kijiji hicho mpaka pale baraza la taifa la hifadhi na usimamizi wa mazingira (NEMC) litakapomaliza uchunguzi wa athari zinazoweza kuwapata binadamu, mifugo na mimea kutokana na matumizi ya maji hayo yanayohisiwa kuwa na sumu.
 
Amesema maeneo ya kijiji hicho zinamoishi kaya tatu zenye watu wapatao 27 yamo ndani ya leseni ya mwekezaji wa kampuni hiyo ya Acacia ambazo hazijahama kutokana na kutokulipwa fidia na baada ya maji hayo kutiririka katika maeneo yao, madhara yaliyopatikana ni pamoja na kukauka kwa mazao na maji  kubadilika rangi.

Ameongeza pia kuwa kutokana na hali hiyo jumla ya wananchi 138 wamepelekwa katika hospiatli ya wilaya ya Kahama kwa uchunguzi huku matokeo ya vipimo yakionesha kuwa hakuna mtu yeyote aliyeathirika na sumu hiyo mbali ya kukutwa na magonjwa mengine ya kawaida.
 
Kwa upande wake afisa usalama wa mgodi wa dhahabu wa Bulyanhulu Abdallah Musika amesema  kufuatia tukio hilo uongozi wa mgodi huo tayari umeimarisha miundombinu ya mabwawa hayo na katika kukabiliana na tatizo la maji kwa wananchi wa kijiji hicho  tayari umepeleka mabomba sita ya maji safi na salama.
 
Hivi karibuni wananchi wa kijiji cha Namba Tisa waliingia hofu kuwa huenda wakapata madhara ya kiafya baada ya kutumia maji ya sumu yaliyoririka kuelekea mashambani na kwenye visima vya maji kutokana na mabwawa yanayotumika kuhifadhia maji hayo ya sumu yaliyotumika kuchenjulia dhahabu kubomolewa na mvua kubwa ya mawe iliyonyesha  kwa takribani nusu saa mfululizo.