Jumatatu , 9th Mei , 2016

Serikali imekiri kuwa adhabu inayotolewa kwa makosa ya vitendo vya rushwa ni ndogo na haiendani na hasara inayosababishwa na makosa hayo hivyo kuwa ni chanzo cha kukwamisha mapambano ya vitendo vya rushwa nchini.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Angela Kairuki.

Akizungumza katika uzinduzi wa Mtandao wa Wabunge wapinga Rushwa, Waziri wa nchi ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Angela Kairuki, amesema kuwa serikali imejipanga kuifanyia marekebisho sheria ya rushwa ili kuondoa mianya hiyo.

Mhe. Kairuki amesema kuwa Serikali na bunge wakiwa ni mihimili mikuu ni lazima wajiepushe na kutuhumiwa dhidi ya kuhusikana na vitendo vya rushwa na kuwa mfano bora wa mapambano dhidi ya rushwa nchini.

Kwa upande wake Spika wa Bunge Mhe. Job Ndugai, akizungumza wakati wa uzinduzi huo amesema kuwa amepata taarifa kutoka tume ya maadili kuwa wanataka kuwasilisha muswada wa sheria ambao utatengenisha ubunge na biashara.

Kwa upande wao wabunge wa Mtandao huo wameitupia lawama Mahakama kwa kuwaachia mafisadi na wengine kufungwa kwa kiwango cha chini hivyo kukwamisha harakati za kupambana na vitendo vya rushwa nchini hivyo wananchi wanakosa imani na Mahakama hizo juu ya maamuzi yao.

Nae Makamu Mwenyekiti wa Mtandao huo, Cecilia Paleso, amesema kuwa kwa wale wabunge ambao wamefikishwa mahakamani na kwa tuhuma za rushwa endapo wakithibitika basi uongozi wa mtandao huo utachukua hatua dhidi yao.

Sauti ya Waziri wa nchi ofisi ya Rais Menejimenti ya utumishi wa Umma na Utawala bora,Bi. Angela Kairuki.
Sauti ya Spika wa Bunge Mhe. Job Ndugai, akielekezea taarifa za Mswada wa tume ya Maadili