Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi wa Kinga kutoka Wizara ya Afya Dkt. Leonard Subi wakati alipotembelea ghala ya kuhifadhia chanjo iliyopo hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma kukagua hali ya chanjo katika mkoa huo.
Dkt. Subi amesema kuwa, chanjo zote aina tisa ambazo zinakinga dhidi ya magonjwa kumi na tatu zipo kwenye ghala hilo. “tulikua na upungufu wa aina mbili za chanjo nchini kati ya tisa ambazo tumekuwa tukizitoa lakini, sasa hivi chanjo zote zipo, kwani zimeshawasili hapa nchini na usambazaji unaendelea”, amesema Dtk. Subi
Hata hivyo Dkt. Subi amesema kuwa, upungufu huo wa chanjo ulitokea baada ya Dunia kukumbwa na janga la mlipuko wa ugonjwa wa COVID-19 ambapo anga zote zilifungwa kwani chanjo husafirishwa kwa mnyororo baridi, kwahiyo huitaji usafiri wa anga.
“Tunamshukuru Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa kulifungua anga la Tanzania ambapo, chanjo sasa zimeanza kuingia nchini na hadi sasa mikoa kumi na tatu(13) chanjo hizi zimeshapokelewa kati ya mikoa 26, na mikoa mingine kumi na tatu ya Tanzania Bara usambazaji unaendelea kupitia Bohari ya Dawa (MSD)”.
Aidha, Dkt. Subi amesema kuwa, usambazaji wa chanjo hizo mbili ambazo wananchi walikua wanazikosa, umeshaanza na watazipata kwa uhakika, huku akielekeza bohari ya dawa nchini (MSD) kuhakikisha chanjo zote zimefika katika mikoa iliyosalia ya Tanzania Bara ifikapo mwishoni mwa wiki hii.