Ijumaa , 3rd Jun , 2022

Waziri wa Mambo ya Nje wa Sweden Ann Linde ameipongeza serikali ya Tanzania kwa hatua mbalimbali inazoendelea kuchukua ikiwemo kuimarika kwa haki za binadamu, uhuru wa vyombo vya habari pamoja na demokrasia

Aidha amesema serikali ya Tanzania imefanya jambo la muhimu kutoa haki kwa wanafunzi wa kike wanaopata ujauzito kuendelea na masomo kwa kutambua elimu ndio nguzo muhimu kwa maisha yao. 

Waziri huyo ameyasema wakati Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Dkt. Philip Isdor Mpango alipokutana na kufanya mazungumzo na waziri huyo leo tarehe 3 Juni 2022 mjini Stockholm nchini Sweden.


Katika mazungumzo hayo Makamu wa Rais wa Tanzania amesema Tanzania na Sweden zimekua na ushirikiano mzuri  wa muda mrefu na serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imelenga kuimarisha uhusiano uliopo baina ya mataifa hayo mawili. 

Aidha ameishukuru serikali ya Sweden kwa kuendelea kuunga mkono jitihada za maendeleo za Tanzania katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya Elimu, Biashara pamoja na  Haki za Binadamu.

Pia Makamu wa Rais amesema serikali ya awamu ya sita inaendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kuboresha mazingira ya uwekezaji, kuimarisha sekta ya viwanda, uhifadhi wa mazingira, kuimarisha sekta ya kilimo pamoja na kuwekeza katika huduma za kijamii kama vile Elimu na Afya. 


Dkt. Philip Mpango yupo nchini Sweden kuhudhuria Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Stockholm +50 wenye lengo la kuchochea utekelezaji wa Malengo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (Ajenda 2030) hususani katika upande wa mazingira na kujadili namna ya kurejesha uchumi endelevu katika kukabiliana na  janga la Uviko 19.