Ijumaa , 10th Nov , 2017

Serikali imekuja na mkakati mpya unaolenga kutokomeza uvuvi haramu, baada ya kuzindua ndege maalum ambayo itakuwa inafanya oparesheni katika eneo la bahari kuu.

Uzinduzi huo wa safari mpya ya ndege umefanywa na Naibu Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega ambapo amebainisha kuwa lengo ni kudhibiti uvuvi haramu katika eneo la bahari kuu.

Ndege hiyo imetua hapa nchini kwa mara ya kwanza kutoka nchini Mauritius kwa ajili ya kufanya doria ya majini. Waziri amesema ujio wa safari hiyo mpya ya ndege ni matokeo ya ushirikiano na nchi za Ukanda wa Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi ili kudhibiti uvuvi haramu kwa njia zote.

“Tumeruhusu ndege ya doria, ili kuongezea nguvu katika njia za kudhibiti wavuvi haramu ambapo awali tulianza kwa njia ya majini kwa kutumia Meli  na sasa ni kwa njia ya anga kwa kutumia ndege hii kutoka Mauritius”.

Aidha Ulega ameeleza kuumizwa na namna ambavyo wavuvi haramu hutumia muda mchache ambao ni chini ya dakika tano kuharibu matumbawe kwa kupiga mabomu kisha athari zake huenda hadi miaka 100.