Jumanne , 12th Jan , 2016

Serikali imetangaza kuwa haitasita kuchukua hatua kali kwa kufunga viwanda, migodi na huduma nyingine za uzalishaji endapo zitabainika kufanya shughuli zao bila kufuata sheria za uhifadhi wa mazingira.

Serikali imetangaza kuwa haitasita kuchukua hatua kali kwa kufunga viwanda, migodi na huduma nyingine za uzalishaji bila kujali zina mchango gani kwa uchumi wa taifa endapo zitabainika kufanya shughuli zao bila kufuata sheria za uhifadhi wa mazingira na vyanzo vya maji nchini.

Kauli hiyo imetangazwa wilayani Tarime mkoani Mara na naibu waziri wa nchi ofisi ya makamu wa Rais muungano na mazingira Luaga Mpina wakati akizungumza na viongozi wa wilaya hiyo, ambapo amesema serikali inatambua mchango mkubwa wa kiuchumi unaotolewa na sekta ya migodi, viwanda na shughuli nyingine za uzalishaji hapa nchini lakini kamwe haitaruhusu shughuli hizo zikinzane na sheria kwa kuruhusu mabaki ya kemikali ya sumu na uchafu mwingine kuharibu vyanzo vya maji.

Katika kikao hicho cha watendaji na viongozi wa serikali wilayani Tarime, naibu waziri huyo nchi ofisi ya makamu wa Rais muungano na mazingira, ametumia fursa hiyo kusisitiza kwa viongozi wa mikoa na wilaya nchini kuwa kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi ni siku ambayo imetangazwa kitaifa ya kufanya usafi wa mazingira na kwamba sheria kali zitachukuliwa kwa viongozi watakaoshindwa kusimamia agizo hilo.

Kuhusu wananchi ambao wamejenga katika maeneo hatarishi ya mabondeni na vyanzo vya maji taratibu zianze kuchukuliwa za kuwaondoa na kuwapa maeneo mengine kabla ya nyumba zao kuvunjwa.

Katika kikao hicho cha pamoja na viongozi wa wilaya ya Tarime, kiongozi huyo amesisitiza kuhusu agizo la serikali la kutaka kila halmashauri nchini kupanda miti milioni moja na laki tano na kwamba zoezi la ukaguzi wa miti hiyo litafanywa kila wakati.