Alhamisi , 3rd Dec , 2015

Serikali imeahidi kuendelea kuwajengea uwezo wajasiriamali wadogo nchini kwa kuwaondolea vikwazo vinavyosababisha mazingira ya kufanyia shughuli zao kuwa magumu.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaama Said Meck Sadiki

Akiongea katika ufunguzi wa maonyesho ya wajasiriamali wa Afrika Mashariki yajulikanayo kama Juakali, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaama Said Meck Sadiki kwa niaba ya Rais John Magufuli amesema serikali imejipanga kuwafanya wajasiriamali kuwa na uwezo wa kuingia katika masoko ya Kimataifa.

Aidha Mh. Sadiki amesema kuwa msuko zaidi kwa sasa ni kuhimiza serikali za afrika mashariki kuzijengea uwezo sekta binafsi kwa ndio kwa sehemu kubwa zinatoa ajira kwa Wananchi.

Kwa upande wake katibu mkuu wa Wizara ya Afrika Mashariki Bi. Joyce Mapunjo amesema kuwa wajasiramali wadogo wakisaidiwa ikiwemo kurasimisha rasimali zao na kuwaingiza katika mifuko ya kijamii wataongeza ajira na kupunguza umasikini nchini.

Katika hatua nyingine imeelezwa kuwa takribani wanawake wajasiriamali elfu nne kutoka nchi tano wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, wameanza kunufaika na mpango wa kuwajengea uwezo wanawake hao, mpango unaolenga kuhakikisha kuwa bidhaa wanazozitengeneza zinapata masoko nje ya ukanda wa Afrika Mashariki na hata ikibidi katika masoko mengine ya kimataifa.

Mpango huo unaratibiwa na taasisi isiyo ya kiserikali ya African Women and Beyond au kwa kifupi AWAB, yenye makao yake makuu nchini Kenya ambapo kwa mujibu wa mmoja wa waanzilishi wake Bw. Joe Kariuki, baadhi ya faida hizo ni pamoja na mbinu mpya za uzalishaji, utafutaji masoko mapya pamoja na namna ya kusimamia biashara zao zisife.

Bw. Kariuki amesema lengo ni kuhakikisha kuwa takribani wanawake elfu kumi wanafikiwa na mpango huo ambao azma yake ni kuwa na kundi kubwa la wanawake wanaomiliki uchumi kupitia biashara na viwanda vidogo vidogo.