Waziri Kivuli wa Fedha na Uchumi katika kambi ya upinzani bungeni Mh. James Mbatia.
Kwa mujibu wa mkurugenzi wa fedha masoko wa Benki kuu ya Tanzania, BOT, Alexnder Ng'winamila amesema kuwa kamwe serikali haiwezi kulifumbia macho suala hilo na kuongeza kuwa endapo serikali itashindwa kudhibiti hali hiyo basi itashindwa kudhibiti na mfumuko wa bei vile vile.
Hatua hiyo imekuja baada ya waziri kivuli wa fedha na uchumi katika kambi ya upinzani bungeni Mh. James Mbatia kutahadharisha serikali pamoja na Benki kuu ya Tanzania kuchukua hatua za haraka za kuzuia kuporomoka kwa shilingi ya Tanzania ambayo mpaka sasa imeporomoka na kufikia asilimia 21.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam jana Mh. Mbatia amezitaja sababu zinazochangia kuporomoka kwa shilingi kuwa ni pamoja na bajeti ya taifa kutegemea wafadhili sambamba na mauzo kidogo kutoka ndani ya nchi kwenda nje ya nchi.
Aidha Mh. Mbatia ameshauri kwamba ili kukabiliana na kuporomoka kwa shilingi ya Tanzania ni lazima sheria za manunuzi ya bidhaa za nje zitiliwe mkazo kwa kuwa kuporomoka huko kwa shilingi kunasababisha athari kubwa kwa watanzania kuendelea na umasikini.