Jumamosi , 7th Feb , 2015

Mkutano wa 18 wa Bunge la Jamhuri ya muungano umemalizika leo kwa bunge kujadili na kupitisha maazimio ya jinsi ya kumaliza migogoro ya ardhi nchini.

Katika maazimio hayo yaliyopokelewa na serikali , serikali imeziagiza mamlaka husika kuwachukulia hatua watendaji wote waliopewa dhamana za uongozi ambao wanasababisha migogoro ya Ardhi, Wakulima na Wafugaji kuendelea na kuifanya kama miradi yao ya kujiingizia kipato katika kufanya usuluhishi.

Akipokea mapendekezo ya kamati teule iliyoundwa kwa ajili ya kuchunguza na kuchambua Sera mbalimbali zinazohusu masuala ya Ardhi, kilimo, Mifugo, Maji na Uwekezaji Waziri Mkuu Mh. Mizengo Pinda amesema Serikali imepokea mapendekezo yote saba yaliyotolewa na kamati hiyo na kuahidi kuyafanyia kazi.

Pinda amesema kuwa Taarifa ya Kamati hiyo imeonesha kuwa migogoro mingi imeshindwa kumalizika kutoka na baadhi ya watendaji kuifanya kama miradi yao ya kiuchumi na kuendelewa kuyagawa makundi ya wakulima na wafugaji.

Katika mkutano huo, jumla ya maswali 122 ya msingi na 313 ya nyongeza yameulizwa na kujibiwa na jumla ya maswali 15 ya msingi na 13 ya nyongeza yaliulizwa na kujibiwa kwa utaratibu wa papo kwa papo kwa Waziri Mkuu.

Mbali na maswali hayo, bunge lilipokea na kujadili taarifa mbalimbali za kisekta na zisizo za kisekta na kupitisha mapendekezo mbalimbali kwa ajili ya kutekelezwa na serikali.

Mkutano huo wa 18 wa Bunge umehitimishwa leo, na Bunge kuahirishwa hadi Tarehe 17 Machi. 2015