Jumamosi , 25th Apr , 2015

Imeelezwa kuwa mabadiliko ya mara kwa mara ya mitaala ya kujifunzia pamoja na kutokuwepo na vitabu vya kiada inachangia kwa kiasi kikubwa vyuo vya ualimu hasa vya binafsi kutokuweza kufanya vizuri.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi nchini Tanzania Mh. Shukuru Kawambwa.

Hali hiyo inatokana na kuwepo kwa uhaba wa vitabu na moduli unaotokana na mihutasari hiyo mipya kutokuambatana na vitabu husika ili kurahisisha ufundishaji kwa vitendo na nadharia.

Rai hiyo imetolewa na mkuu wa chuo cha uwalimu Kange kilichopo jijini Tanga Joel Mchome wakati wa mahafali ya tisa ya ngazi ya cheti ya walimu wa Grade A hapo jana.

Amesema kuwa hali hiyo inachangia kushuka kwa kiwango cha elimu kinachotolewa hivyo kuchangia kutopatikana kwa walimu bora au wanachuo kutumia muda mwingi kutafuta mitaala hiyo.

Aidha mkuu huyo wa chuo ameiomba serikali kutoa msaada kwa vyuo binafsi ili kupunguza gharama kwa wanafunzi na wazazi ambao hawamudu gharama za vyuo binafsi.