Jumanne , 19th Aug , 2014

Wakala wa Jiolojia Tanzania GST umeitaka serikali kusitisha usafirishaji wa madini ghafi nje ya nchi ili kuwanufaisha zaidi wananchi na kuongeza pato la taifa.

Akizungumza jana jijini Dar es salaam Mtendaji mkuu wa GST,Prof Abdulkarim Mruma amesema kuwa Watanzania wana haki ya kunufaika na rasilimali za madini,mafuta na gesi zilizogunduliwa nchini katika maeneo mbalimbali.

Prof. Mruma ameitaka serikali kuwekeza zaidi katika uendelezaji wa sekta ya madini kwa kuziongezea uwezo Taasisi zinazosimamia sekta hiyo kwa lengo la kubadilisha mwenendo uliopo.

Ameongeza kuwa serikali izuie kabisa uuzaji wa madini ghafi nje ya nchi ili uongezaji wa thamani ufanyike nchini utasaidia kuwanufaisha zaidi wananchi kwa kuongeza ajira na pato la taifa kupitia viwanda.

Wakati huo huo, Waziri mkuu Mizengo Pinda amesema serikali inakusudia kuboresha zaidi mtandao wa barabara maeneo ya vijijini hasa zile zilizo katika maeneo yenye uzalishaji hususani kilimo ili kuhakikisha barabara hizo zinapitika katika kipindi chote cha mwaka.

Waziri Mkuu Pinda amesema hayo katika mkutano wa siku Nne uliowakutanisha wadau mbalimbali wa barabara wakiwemo wahandisi,wakuu wa mikoa na kuongeza kuwa zaidi ya asilimia 60 ya barabara za halmshauri zimejengwa kupitia mfuko huo.

Kwa upande wake mwenyekiti wa bodi ya mfuko wa barabara James Wanyancha amesema kwa sasa bodi hiyo inakabiliwa na changamoto kubwa ya ucheleweshwaji wa fedha kutoka wizara ya fedha jambo linalochangia kuchelewa kwa utekelezaji wa miradi hiyo kwa wakati.