Jumatano , 6th Jul , 2016

Serikali imetakiwa kubuni mbinu mbadala zitakazo wezesha nchi kuzalisha na kujitosheleza kwa kuwa na wataalamu waliobobea kwenye sekta ya uhasibu, masoko na biashara ili kuweza kusimamia shughuli za maendeleo ya viwanda nchini.

Hayo yamesemwa na Msemaji wa Chuo cha Elimu ya Biashara cha (CBE) Bw. Leonidas Tibanga wakati akiongea na East Africa Radio leo jijini Dar es Salaam na kusema kuwa mikakati ya kupata wataalamu hao iendane na kasi ya kuanzisha viwanda.

Bw. Tibanga amesema, kwa sasa chuo cha CBE kimeanzisha shahada ya uzamili kwenye sekta ya usimamizi wa biashara kimataifa pamoja na usimamizi wa ununuzi na ugavi kimataifa ili kuweza kuzalisha watalimu wa kufundisha masomo ya biashara na uhasibu katika shule za sekondari nchini.

Naye Mkufunzi wa Chuo hicho Bw. Faraja Edward amesema kwa sasa kuna uhaba mkubwa wa wataalamu wa vipimo na mizani nchini hali ambayo itapelekea serikali kukosa mapato hasa katika sekta ya gesi ambayo faida yake inategemea vipimo sahihi kwa wanunuaji wajumla na rejareja.