Jumatatu , 29th Feb , 2016

Wamiliki wa Viwanda nchini wameiomba serikali itatue kero ya upatikanaji wa nishati ya umeme pamoja na uingizwaji wa bidhaa nchini zisizotozwa kodi jambo linaloathiri viwanda vya ndani na kushindwa kuhimili ushindani.

Naibu Waziri wa Muungano na Mazingira,Luhaga Mpina

Hayo yameelezwa na mmiliki wa kiwanda cha Lodhia , amesema kuwa iwapo serikali ina nia ya dhati ya kukuza viwanda vya ndani haina budi kuvilinda viwanda hivyo kwa kuzuia na kudhibiti uingizwaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi.

Naibu Waziri wa Muungano na Mazingira, Luhaga Mpina amesema kuwa serikali itaendelea kujenga mazingira bora kwa ajili ya viwanda ili kukuza ajira na uchumi wa nchi kwa ujumla ikiwemo kutatua matatizo ya nishati.

Katika ziara ya Naibu Waziri huyo ambaye alitembelea kiwanda cha nguo cha A TO Z amekitaka kiwanda hicho kulipa faini ya shilingi milioni 70 waliyowekewa na Baraza la Mazingira la NEMC kwa kuchafua mazingira kwani endapo watashindwa kulipa kwa siku 7 watachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufungiwa kiwanda.

Naibu Waziri wa Mazingira amefanya ziara yake jijini Arusha ambapo alitembelea soko kuu la Arusha, machinjio ya Arusha Meat, kiwanda cha Sanlfag pamoja na kiwanda cha chuma cha Lodhia lengo ikiwa ni kuangalia athari za kimazingira zinazosababishwa na viwanda na jinsi ambavyo wanaweza kukabiliana na athari hizo kwa kutumia miundombinu ya kisasa ili kupunguza athari.