Alhamisi , 17th Dec , 2015

Serikali imeshauriwa kutumia taarifa zinazotokana na uwekezaji wa miradi ya rasilimali za mafuta na gesi kupanga mipango ya maendeleo ya wananchi, ili waweze kufaidika na uwekezaji huo unaotekelezwa katika maeneo mbalimbali katika mikoa ya Kusini.

katibu mtendaji wa Shirika la Faidika Wote Pamoja (FAWOPA), Komba Bartazar

Hayo yamezungumzwa mkoani Mtwara na katibu mtendaji wa Shirika la Faidika Wote Pamoja (FAWOPA), Komba Bartazar, katika ufunguzi wa mafunzo ya siku tatu ya kuwajengea uwezo watendaji wa serikali za mitaa, vijiji na kata pamoja na vijana, juu ya namna watakavyoweza kuwahamasisha wananchi kushiriki katika uchumi wa gesi na mafuta.

Amesema, mkoa wa Mtwara sasa unaelekea katika uwekezaji mkubwa wa uchumi wa rasilimali hizo huku wananchi wake wakiwa bado hawajawa na taarifa za kutosha kuhusiana na sekta hiyo ambayo ni mpya mkoani humo na nchini kwa ujumla.

Aidha, amesema kupitia mafunzo hayo ambayo yamefadhiliwa na shirika la OXFARM la nchini Marekani, watendaji hao na vijana wataweza kuelewa namna ya kwenda kuwafundisha wananchi juu ya sera ya ushiriki wa wazawa na biashara zao katika michakato ya miradi ya gesi na mafuta.