Jumatano , 5th Jun , 2024

Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa amesema sekta ya Usafiri wa Anga Barani Afrika imekuwa ikipiga hatua kusonga mbele huku akisema bado juhudi za Pamoja zinahitajika ili kuongeza kasi ya ukuaji wake.

Prof. Makame Mbarawa

Mbarawa amesema hayo wakati akifungua mkutano wa wakuu wa taasisi za Usafiri wa Anga Afrika jijini Arusha, ambao wanakutana kujadili kwa Pamoja namna bora ya kuboresha sekta ya Usafiri wa Anga Barani Afrika.

Amesema mkutano huu ni muhimu sana na unafanyika wakati sahihi ambapo uelewa wa wananchi wengi juu ya Usafiri wa anga umeongezeka.

"Ni heshima kwetu kama nchi kupata fursa ya kuandaa mkutano huu, sina shaka kuwa mtajadili na kufanya maamuzi sahihi kwa maslahi ya bara letu la Afrika" amesema Prof. Mbarawa

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania Bw. Hamza Johari amesema mkutano huu siyo tu unawakutanisha wakuu wa taasisi kujadili utatuzi wa changamoto bali ni kuwa na sauti ya Pamoja kama Afrika katika majukwaa ya kimataifa ili kuhakikisha maslahi ya Afrika yanazingatiwa.

Mkutano huu wa pili unafanyika kwa siku mbili kuanzia Juni 5 - 6, jijini Arusha na wajumbe watapata nafasi ya kutembelea hifadhi ya Ngorongoro ikiwa ni sehemu ya kukuza utalii nchini.