
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega
Waziri Ulega ametoa rai hiyo wakati akifungua warsha kuhusu uzalishaji wa protini kwa ajili ya vyakula vya mifugo na kupunguza ushindani iliyofanyika jijini Dar es Salaam Septemba 29, 2023.
Amesema kuwa tasnia hiyo imepewa kipaumbele na umuhimu wa pekee kwa kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi imetunga sheria mahususi inayojulikana kwa jina la Sheria ya Maeneo ya Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Wanyama (Sura Na.180) pamoja na Kanuni na Miongozo mbalimbali, ambapo lengo la sheria hiyo ni kuhakikisha vyakula vinavyozalishwa vinakidhi ubora na viwango stahiki ili kuwezesha uzalishaji bora wa mifugo, samaki na mazao yatokanayo na mifugo na samaki.
"Hivyo, ninapenda kupitia warsha hii kutoa rai na msisitizo mkubwa kwa wazalishaji wa vyakula vya mifugo wote nchini kuhakikisha wanapeleka sampuli za vyakula wanavyozalisha kwenye maabara ya TVLA ili kuhakiki ubora na viwango kwa kuzingatia matakwa ya sheria hiyo kabla ya kuanza kuwauzia wafugaji wetu au kuvisafirisha nje ya nchi," amesema Waziri Ulega
Aliendelea kufafanua kuwa pamoja na Sheria hiyo, Wizara inayo Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) iliyopewa jukumu la kuhakiki na kupima ubora na viwango stahiki vya malighafi zinazotumika kwenye uzalishaji wa vyakula vya mifugo.
Aidha, ameitaka TVLA kuhakikisha inatembelea katika maeneo ya wazalishaji wa malighafi za kutengeneza vyakula vya mifugo ili wakakague ubora wa malighafi hizo ili kuongeza tija na ufanisi wa kazi katika kulinda usalama wa chakula cha mifugo.
Sambamba na hilo, Waziri Ulega amewahimiza wafugaji wote wa mifugo na samaki na watumiaji wa rasilimali za vyakula vya mifugo, kuhakikisha wanatumia vyakula vinavyozalishwa kwenye viwanda vilivyosajiliwa na kutambuliwa rasmi na Wizara ya Mifugo na Uvuvi.
Kwa upande wake, Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania, Wieber de Boer amesema gharama za uzalishaji wa protini kwa ajili ya chakula cha mifugo ni kubwa hapa nchini hivyo wapo tayari kushirikiana na serikali ya Tanzania katika kutafuta njia mbadala ya kutatua changamoto hiyo ili sekta ya mifugo iweze kukua vizuri.