Alhamisi , 7th Apr , 2022

Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameshiriki katika maadhimisho ya kumbukizi ya kifo cha Rais wa kwanza wa Zanzibar Marehemu Abeib Amani Karume katika ofisi za makao makuu ya chama cha mapinduzi (CCM) Kisiwandui Unguja visiwani Zanzibar.

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, akiwa na baadhi ya viongozi katika maadhimisho ya kumbukizi ya Marehemu Karume

Katika kumbukizi hiyo vijana wametakiwa kuwa wazalendo kwa taifa lao kama njia ya kumuenzi Rais Karume, aliyehimiza uzalendo, umoja na mshikamano katika enzi za uongozi wake.
Akizungumza na EATV mchambuzi wa masuala ya siasa Severine Kapinga amebainisha kuwa uzalendo wa Marehemu Karume ndio uliochochea mapinduzi matukufu ya Zanzibar na baadaye kuleta umoja visiwani Zanzibar.
"Bila Rais Karume na wenzake kuamua kuunganisha Tanganyika na Zanzibar, hii leo zingekuwa nchi mbili tofauti, vijana tujifunze uzalendo, umoja na mshikamano kupitia maisha ya Rais Karume.'' Amesema Severine Kapinga, Mchambuzi wa masuala ya kisiasa.
Kwa upande wake Ally Suleiman Khalid kutoka Zanzibar ameeleza kuwa Muuungano wa Tanganyika na Zanzibar ni moja ya matunda ya juhudi za Hayati Karume, Mwalimu Nyerere na viongozi wengine, hivyo akawataka Watanzania kuendelea kuulinda Muungano huo.
Viongozi wengine walioshiriki katika maadhimisho hayo ni pamojana Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango, Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Mwinyi pamoja na Rais mstaafu wa Zanzibar Amani Abeid Karume.