Kamanda wa Polisi Singida Sweetbert Njewike
Akizungumza leo Februari 28, 2020 na EATV&EA Radio Digital, kamanda Njewike amesema kuwa walioitoa taarifa hiyo hawakumnukuu vizuri kwani yeye hakutoa taarifa ya moja kwa moja kuwa Jonas hakuwa kiongozi wa CHADEMA.
"Nilichosema kwamba yule ni bodaboda inawezekana anafanya kazi nyingine, sikukanusha kwamba yule siyo kiongozi wa CHADEMA, naomba mninukuu vizuri na ndicho nilichokisema" amesema Kamanda Njewike.
Kwa mujibu wa Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema, kupitia ukurasa wake wa Twitter ameandika kuwa Alex Joas alikuwa ni Katibu wa CHADEMA Manyoni Mashariki.
Alex Joas inadaiwa kuwa mwili wake uliokotwa mbugani mbali na barabarani, ukiwa na majeraha ya kuchomwachomwa na kitu chenye ncha kali na kwamba Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi ili kubaini nani aliyehusika na mauaji hayo.

