Ijumaa , 23rd Jul , 2021

Mkuu wa mkoa wa Arusha John Mongella, amesema kuwa kuanzia sasa mikusanyiko isiyo halali mkoani humo itadhibitiwa na kuwataka wananchi kuachana na mikusanyiko hiyo kwa lengo la kujiepusha na maambukizi ya virusi vya Corona.

Mkuu wa mkoa wa Arusha John Mongella

Kauli hiyo ameitoa wilayani Arumeru na kuongeza kuwa mikusanyiko yote itafuata utaratibu wa kibali na ile mikusanyiko ya misiba na mazishi wana ndugu wajipange na kwamba isiwe sababu ya kuongeza maambukizi.

"Niseme kwa sasa mikusanyiko itadhibitiwa na hatutaruhusu mikusanyiko isiyokuwa na sababu za msingi naomba hili lisichukuliwe kama ni suala la mkuu wa mkoa hili tulichukue wote kama jamii ili tuweze kujilinda, maendeleo yote haya tunayohubiri au kuyatangaza hayana maana kama tutakuwa na jamii yenye afya yenye mgogoro, au tunapoteza muda mwingi kwenye misiba na kuuguza ndugu zetu," amesema RC Mongella.

Kufuatia kauli hiyo Jeshi la Polisi mkoani Arusha limesema kwamba limepokea maelekezo hayo na kwamba wote watakaofanya mikusanyiko hiyo hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.