Rais Jakaya Kikwete
Leo tunaanza mwanzo mpya katika historia ya uhusiano baina ya Watanzania waishio ughaibuni na Watanzania waishio nchini. Kwa mara ya kwanza tunawakutanisha hapa nchini Watanzania waishio ughaibuni na Watanzania wenzao na taasisi zetu za hapa nchini. Toka tumeanza kampeni hizi za kuhamasisha Watanzania waishio nje kushiriki katika maendeleo hapa nchini, hatujawahi kuwa na mkutano kama huu. Tumefanya mikutano mingi nje ya nchi ya kuwatembelea huko mliko, kuzungumza nanyi na kuwahamasisha kushiriki katika shughuli za ujenzi wa taifa. Safari hii, ni kinyume chake. Mmekuja nyumbani kujumuika nasi. Hii ni hatua kubwa na mwanzo mpya.
Nakupongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa kuliwezesha jambo hili kuwa. Nawashukuru kwa jitihada mnazochukua kusaidia kusukuma agenda hii ya Diaspora na maendeleo. Matunda haya ya leo ni matokeo ya kazi yenu nzuri. Nakupongeza pia Ndugu Emmanuel Mwachulla na wenzako kwa kubuni wazo hili jema, na kuishirikisha Serikali katika kulifanikisha. Uamuzi wenu wa kulianzisha wazo hili ni mzuri kwani unaondoa ile dhana kuwa suala hili la Diaspora ni suala la sisi viongozi tu na siyo agenda yenu. Kujitokeza kwenu kunatutia nguvu na moyo wa kuendelea kuhamasisha. Ni ukweli usiopingika kuwa sauti yenu katika suala hili la ushirikishaji wa diaspora ina uzito mkubwa zaidi kuliko hata sauti yetu sisi.
Kauli Mbiu ya Mkutano
Mabibi na Mabwana;
Nimevutiwa na kauli mbiu ya mkutano huu “Connect, engage, inform and invest”, yaani unganisha, wasiliana, toa habari na wekeza”. Kuwafikia wana diaspora ilikuwa ni moja ya malengo makuu ya Serikali yetu kwa sababu tunaamini kuwa jukumu la maendeleo ya Tanzania ni la kila Mtanzania po pote pale alipo. Ndugu zetu walioko nje nao kama walivyo waliopo nchini wana wajibu wa kuchangia pia kwa kile wanachokiweza. Nilipokuwa nakutana na Watanzania kote nilikopita nje ya nchi nilifafanua mambo matatu muhimu kwa Watanzania: La kwanza ni kukumbuka nyumbani (East West Home is Best). La pili, wajenge nyumbani na wasaidie ndugu zao, na la tatu wasaidie maendeleo ya nchi kwa kuleta vitega uchumi, kutafuta masoko ya bidhaa, walete teknolojia na walete ujuzi na maarifa.
Umuhimu wa Diaspora kwa Uchumi wa Taifa
Mabibi na Mabwana;
Umuhimu wa Diaspora katika uchumi wa nchi zao za asili ni suala ambalo limepewa mkazo sana katika dunia ya leo. Inakadiriwa kuwa watu wapatao milioni 220 duniani ambao ni asilimia 3 ya watu wote duniani wanaishi nje ya nchi zao za asili. Benki ya Dunia imebaini kuwa, kiasi cha dola za Marekani bilioni 581 zimetumwa na Wana-Diaspora duniani kote kwenda kwenye nchi zao za asili mwaka 2013. Kiasi hiki kinatarajiwa kuongezeka kufikia dola za Marekani bilioni 681 ifikapo mwaka 2016. Nchi zinazoendelea zinatarajiwa kupata ongezeko la asilimia 78, za fedha hizi kutoka dola za Marekani bilioni 404 mwaka 2013 hadi dola bilioni 516 mwaka 2016. Kiasi hiki cha sasa kinakadiriwa kuwa ni mara nne ya fedha ambazo nchi za Afrika zinapokea kama misaada kutoka kwa wafadhili wa nje. Itoshe tu kusema kuwa diaspora ni chanzo muhimu cha kuchangia kukuza uchumi wa nchi.
Pamoja na ukubwa wa mapato hayo, bado Tanzania inavuna kiasi kidogo sana kutoka kwa Watanzania waishio nje. India na China peke yake zinavuna jumla ya kiasi cha dola za Marekani bilioni 50 kwa mwaka, na Nigeria kiasi cha dola bilioni 21 katika mwaka 2013. Kwa mujibu wa Ripoti ya UNCTAD ya mwaka 2012 kuhusu ushirikishwaji wa diaspora, inakadiriwa kuwa Tanzania ilipokea kiasi cha dola za Marekani milioni 10.2 tu (sawa na shilingi bilioni 16) mwaka 2011. Kwa ulinganisho wao, kiasi cha dola za Marekani milioni 4.5 zilitoka kwa Watanzania waishio Uingereza, dola milioni 3.2 kwa wale waishio Canada na dola milioni 2.5 kwa wale waishio Kenya, ingawa takwimu hizi hazihusishi fedha zilizorejeshwa nchini kwa njia zisizo rasmi bado. Kiasi hiki ni kidogo sana ikilinganishwa na Kenya iliyopata dola za Marekani bilioni 1.3 mwaka 2014.
Changamoto kubwa tuliyonayo nchini ni kutokuwepo na takwimu rasmi za kiasi cha fedha tunachopokea kutoka nje kutokana na fedha nyingi kupita katika mikondo isyo rasmi ya fedha. Naamini kuwa tukiweka mufumo yetu sawa upo uwezekano mkubwa wa kiwango hiki kuongzeka.
Hapana shaka ipo fursa ya Tanzania kuvuna zaidi kutoka kwa Diaspora yake. Hapana shaka pia kwamba ili tuweze kufanikiwa hatuna budi kuwekeza katika kuweka mazingira mazuri ya kisera na kisheria. Hatuna budi kuondoa vikwazo vinavyowazuia Diaspora wetu kushiriki ujenzi wa taifa. Maana uzoefu umeonyesha pale ambapo mazingira ni wezeshi, michango ya Diaspora imekuwa ni mikubwa zaidi. Mfano, Diaspora wa Salvador wanakadiriwa kutuma nyumbani kwao asilimia 16 ya mapato yao binafsi, Bangladesh na Philippines ni asilimia 12 na Senegali ni asilimia 9.
Mabibi na Mabwana;
Sisi katika Serikali tumechukua hatua kubwa katika kurekebisha hali hii ili kujenga mazingira wezeshi. Ilani ya uchaguzi wa CCM ya mwaka 2005 na ile ya 2010 ilitoa maelekezo mahsusi kuhusu kutambua na kuweka mazingira mazuri ya kuwezesha diaspora kuchangia maendeleo ya nchi yetu. Tumeunda Idara ya kushughulikia Diaspora ndani ya Wizara ya Mambo ya Nje, tumeunda nafasi ya uratibu ndani ya Ofisi ya Waziri Mkuu, tumefanya kampeni kubwa ya kuhamasisha wadau wa ndani kutambua na kushirikisha diaspora, na nimetumia kila fursa nilipotembelea nje kukutana nanyi na kuwahamasisha kuchangia maendeleo ya nchi. Aidha, tumewashirikisha diaspora katika mchakato wa Katiba mpya.
Matokeo ya jitihada hizi yameanza kuonekana, ndiyo maana kumekuwepo na ongezeko la fedha zinazotoka Diaspora kama takwimu zinavyoonyesha. Aidha, taasisi za fedha, taasisi za nyumba na mifuko ya jamii nayo imesikia wito huu na wameanza kutoa huduma mahsusi kwa Watanzania walioko nje na watu wenye asili ya Tanzania waishio nje ya nchi. Ni dhamira yetu kuona huduma hizi zikipanuka na kuboreshwa siku hadi siku. Serikali iko katika hatua za kukamilisha sera ya diaspora itakayoshirikisha na kuunganisha juhudi za wadau wote katika kuweka mazingira mazuri kuwezesha ushiriki wenu kwa ukamilifu.
Madai ya Uraia Pacha
Mabibi na Mabwana;
Ninapokutana nanyi huko nje na hivi majuzi nilipokuwa Washington D.C na Houston, Texas, kilio chenu kikubwa ni kupitishwa kwa haki ya Mtanzania wa kuzaliwa kutopoteza uraia wake iwapo atapata uraia wan chi nyingine. Suala hili ni la kikatiba na si la mamlaka ya Rais pekee. Katika Rasimu, suala la Uraia limefafanuliwa katika Sura ya 5 ya Rasimu ya Tume, Ibara ya 59 inazungumzia Hadhi ya watu wenye asili au nasaba ya Tanzania. Yamekuwepo maoni kutoka kwenu kuwa, Ibara hii ilivyowekwa haijakata kiu yenu ya kutaka kuendelea na kuwa na haki ya kutopoteza uraia wa asili wa Tanzania. Mnasema kwamba pamoja na kuwa pendekezo la kupewa “Hadhi” si haba, bado hadhi hiyo sio mbadala wa uraia wa asili.
Mimi nilitimiza ahadi yangu kwenu kwa kuteua Mjumbe mmoja kutoka Diaspora, Bw. Kadari Isingo ili awawakilishe kwenye Bunge la Katiba. Ni juu yenu kumtumia vizuri na pia kuelimisha umma juu ya dai lenu hili. Katika hilo la Uraia, mtumie ushawishi uleule, mpaze sauti vilevile kama mnavyofanya katika mitandao ya jamii kwenye masuala mengine.
Matarajio ya Watanzania Walioko Nchini
Mabibi na Mabwana;
Watanzania walioko hapa nyumbani wanayo matarajio makubwa kutoka kwenu. Wanayo imani kuwa, kwenda kwenu nje kuhemea kutaongeza neema kwenye familia zenu na taifa kwa ujumla. Wanatazamia kuwa maisha yenu huko nje ni bora zaidi na mmekwenda kuvuna ili mjenge na kuendeleza kwenu. Wanategemea mkiwa huko mtawasaidia ndugu zenu kutatua changamoto za maisha. Muonapo fursa za kusaidia maendeleo nchini mtazileta. Mtaleta fedha, mtaleta vitega uchumi, teknolojia za kisasa pamoja na ujuzi na maarifa. Mkiona fursa za ajira mtawasaidia na wenzenu wapate. Kwa wale waliopata bahati ya kupata ujuzi mzuri, tungependa kuwaona mkiutumia ujuzi huo na maarifa yenu kuendeleza kwenu. Kunapotokea nafasi za ajira jitokezeni kuomba. Najua hatuwezi kuwalipa mishahara mikubwa kama ya huko mliko lakini penye utashi wa kuchangia maendeleo kiasi cha mshahara si kigezo pekee.
Ahadi ya Serikali
Mabini na Mabwana;
Sisi katika Serikali hatutarudi nyuma katika azma yetu na kuendelea kuwashirikisha katika maendeleo yetu hapa nchini. Tunayo kila sababu ya kufanya hivyo na tayari tunafanya hivyo. Tutaimarisha sera, mifumo na sheria ili kuweka uwanja wazi wa kuwawezesha kuchangia maendeleo ya hapa nchini. Tunataka mtumie mifumo rasmi na salama ya kutuma fedha, kumiliki mali na kushiriki katika mifumo ya kiuchumi. Hii itawaepusha na hasara mnazoweza kupata pale mnapojaribu kuwekeza nyumbani kwa kutumia fedha kwa njia zisizo rasmi kupitia kwa ndugu, jamaa na marafiki. Nafurahi kwamba katika mkutano huu mtapata nafasi ya kuelezwa yale tuliyopanga kufanya na tunayofanya kwa ajili hiyo. Zitumieni fursa hizo.
Hitimisho
Mbibi na Mabwana;
Nawapongeza tena kwa mwitikio wenu mkubwa na zaidi kwa kufanya mkutano huu nchini. Mmedhihirisha tena ule usemi wetu wa Kiswahili wa “mtu kwao”. Tunafarijika sana mnapotuonyesha kuwa mnakumbuka nyumbani kwenu. Jisikieni kuwa mko nyumbani na muwe huru kuja wakati wote maana “mwenda kwao si mtoro” sisi tunawapokea kwa mikono miwili maana ninyi ni watoto wa nyumbani. Pendeni kwenu, “mkataa kwao mtumwa”.
Asanteni kwa kunisikiliza.