Jumatano , 20th Oct , 2021

Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye, anatarajiwa kuwasili nchini kwa ziara ya kitaifa ya siku tatu itakayoanza Oktoba 22 hadi 24 mwaka huu ambapo atapokelewa na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Rais wa Burundi, Evariste Ndayishimiye

Katika ziara yake hiyo Rais Ndayishimiye ataweka jiwe la msingi katika kiwanda cha kuzalisha mbolea ya asili yenye mchanganyiko wa madini ya phosphate na samadi kinachojengwa katika eneo la viwanda la Nala, Jijini Dodoma kiwanda ambacho kinajengwa na wawekezaji wa kampuni ya Itracom Fertilizers Limited (ITRACOM) kutoka nchini Burundi.

Mnamo Oktoba 23 Rais Ndayishimiye ataelekea Zanzibar ambako atapokelewa na Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Mwinyi, na kuwa na mazungumzo na mwenyeji wake huyo na baadaye atarejea Jijini Dar es Salaam ambapo ataungana na mwenyeji wake Mhe. Rais Samia.

Mbali na hayo akiwa Dar es Salaam Rais Ndayishimiye anatarajiwa kutembelea Bandari ya Dar es Salaam na kukagua ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR unaoendelea nchini kutokea stesheni ya Dar es Salaam hadi stesheni ya Kwala - Ruvu pamoja na kutembelea bandari kavu ya Kwala inayojengwa na Mamlaka ya Bandari Tanzania katika eneo hilo.