Akiongea na EATV baba mzazi wa wa mtoto huyo Mohamedi Nasoro, amesema ameamua kuendeleza ndoto ya mtoto wake huyo, ambaye anaeleza kuwa akiwa na umri wa mwaka mmoja na miezi minne, alimsikia mtoto huyo akisema anataka kuwa rais, hivyo kuamua kumuendelezea ndoto zake huyo.
"Huyu mtoto alipofikisha umri wa mwaka mmoja na miezi minne alitamka kwa akili yake mwenyewe akisema nataka kuwa rais, kwa hiyo sikuona ajabu ni kwa nini huyu mtoto alitamka hivyo, kwa sababu nimeona mambo mengi kuna watu wanazaliwa na vitu vikubwa, kina sheikh Sharif, basi nikaona hiki ni kipaji chake, mimi nikanza kumuwekea lengo kama alivyosema nataka kuwa rais, nikaanza kuendeleza kipaji chake cha urais", alisema baba wa mtoto huyo.
Mzee huyo mwenye umri wa miaka 67 aliyetokea mkoani Singida akiwa na baiskeli aliyoitengenezea sehemu maalum ya kukaa na jukwaa kwa ajili ya mtoto wake huyo, huku ikiwa imepambwa rangi za chama cha Mapinduzi (CCM), amesema ameamua kuja Da es salaam ili kuonana na Rais Magufuli, ili aweze kumsaidia katika kufanikisha ndoto za kijana wake.
Mzee Nasoro ambaye amekiri kuwa mwanachama wa CCM (kada) amesema ameamua kumuingiza kwenye chama hicho mtoto wake, ili akue huku anakijua chama chake, kwani hawezi kumfundisha taratibu za mtu mwengine tofauti na zake.
"Mimi siwezi kumfundisha tabia za mtu mwengine au za jirani yangu, namfundisha tabia yangu, na ndio maana nikaamua chama ninachokiabudu, ndicho hicho hicho nitakacho mfundisha nacho, kitu ninachokwenda kwa Raisi na ninachotaka anisaidie kama ataamua kunisaidia, ni kumuendeleza kwenye shule za vipaji, ili mtoto wangu asome ", alisema Mzee Nasoro ambaye ndiye baba mzazi wa mtoto Yusuph.
Mzee Nasoro amesema iwapo vyama vingine vitamuhitaji mtoto wake kugombea urais kipindi hicho hataruhusu, kwani mtoto wake huyo ni mwanachama wa chama cha mapinduzi.(Kumbuka kwa sasa mzee huyo ana miaka 67, na mpaka 2050 atakuwa na miaka 101, ni kudra za Mwenyezi Mungu tu kama atakuwepo mwaka huo na kumkataza mtoto wake asiende chama kingine)
Mzee Nasoro ambaye ana watoto watano na Yusuph ndiye mtoto wake wa mwisho, anajihusisha na biashara ya chakula (mgahawa), pia amesema yeye ni muathirika wa Virusi vya ukimwi (VVU) tangu mwaka 1992, na mpaka sasa hatumii dawa zozote, ila anatumia chakula bora ili kuweza kujikinga.
Mzee Nasoro amesema anaamini mtoto wake huyo atatimiza malengo yake ya kuwa rais, na iwapo hatakuwa rais basi atakuwa kiongozi yoyote wa ngazi za juu.
"Naamini kwamba atafikia kwa sababu hiyo ni ndoto yake, atapigana kufa na kupona, na kama hatafikia hivyo basi ni bora awe kiongozi wa juu, waziri mkuu, makamu wa rais", alisema Mzee Nasoro.




