Ijumaa , 9th Aug , 2019

Rais wa Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed Shein amezitaka Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuweka mkazo wa matumizi ya bidhaa zake na wataalamu wake wa ndani katika kutengeneza fursa za ajira na masoko.

Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein, akiwa katika picha ya Pamoja na Viongozi (SADC).

Akizungumza katika hafla ya kufunga Maadhimisho na Maonesho ya Nne ya Wiki ya Viwanda katika Nchi za SADC Jijini Dar es Salaam, Rais Shein alisema umefika wakati kwa mataifa hayo kuzalisha bidhaa bora zenye kuweza kuleta ushindani katika masoko ya ndani na nje ya Jumuiya hiyo.

Dkt. Shein alisema Mataifa ya SADC hayana budi kutumia fursa ya maonesho hayo katika kutangaza fursa za ujuzi na ubunifu kwa kuzalisha na kutengeneza mtandao wa imara wa mawasiliano baina ya Nchi hizo na kuweza kuwa na soko la pamoja litakalowawezesha kutengeneza fursa za ajira kwa wananchi wa Mataifa hayo.

Dkt. Shein aliongeza kuwa ili kufikia malengo ya uzalishaji wa bidhaa bora za viwandani ni wajibu wa Serikali zote kutengeneza mtandao imara wa miundombinu ikiwemo matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano kwa kuunda mikakati ya pamoja ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Jumuiya hiyo uliolenga katika kuimarisha sekta ya viwanda ndani ya jumuiya hiyo.

“Hatujakataa mchango wa wataalamu na bidhaa za nje, lakini chako ni chako na mwenzako si chako, hivyo akikunyima usikasirike, ni wakati wetu sasa kuweka mkazo katika kutegemea wataalamu wetu na teknolojia zetu katika uzalishaji wa bidhaa zetu” alisema Dkt. Shein.

Aliongeza kuwa Nchi za Jumuiya hiyo hazina budi kutumia fursa za Maonesho na midahalo mbalimbali ya wataalamu inayojadiliwa katika Mikutano ya Jumuiya hiyo ili kuweza kubaini changamoto na hatua mbalimbali zinazopaswa kuchukuliwa ili kuiwezesha jumuiya hiyo kupiga hatua kubwa za Maendeleo ikiwemo kutengeneza fursa za ajira kwa wananchi wake.