Jumamosi , 8th Jul , 2023

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuhudhuria na kuhitimisha maadhimisho miaka 60 ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) yatakayofanyika kitaifa uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.

Akizungumza na waandishi wa habari ukumbi wa idara ya Habari Maelezo, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Innocent Bashungwa amesema maadhimisho hayo yatafanyika Julai 10 mwaka huu ikiwa ni siku maalum ya miaka 60 ya tangu kuanzishwa kwa jeshi hilo.

“Siku ya kilele pamoja na mambo mengine wananchi watashuhudia kazi mbalimbali zinazofanywa na vijana wa JKT ikiwamo michezo mbalimbali na ngoma za utamaduni, Rais Samia atashuhudia hayo yote,” Amesema Waziri Bashungwa.

Aidha, Bashungwa amesema katika miaka 60 jeshi hilo limefanikiwa kutekeleza majukumu mbalimbali ya kimsingi ikiwamo ulinzi pamoja na malezi ya vijana katika kuwajengea uzalendo.
Katika kuelekea kuadhimisha miaka 60 ya jeshi hilo limefanikiwa kufanya shughuli mbalimbali za kijamii zikiwamo za kutoa msaada kituo cha taifa cha watoto yatima Kikombo na kufanya usafi maeneo mbalimbali.