Jumapili , 27th Jun , 2021

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suhulu Hassan, amewataka Watanzania kuendelea kuchukua tahadhari ya ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suhulu Hassan

Rais Samia ametoa ujumbe huo leo Jumapili Juni 27, 2021, kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii ambapo amewataka kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni, kutumia vitakasa mikono, kuvaa barakoa na kutokugusana akisisitiza kuwa  ugonjwa huo upo.

“Nawasihi watanzania wenzangu tuendelee kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Korona (Uviko-19) kama tunavyoelekezwa na wataalamu wetu wa afya. Tunawe mikono kwa maji tiririka na sabuni, tutumie vitakasa mikono, tuvae barakoa na tusigusanegusane. Ugonjwa wa Korona upo,” ameandika.

Ujumbe huo wa Rais Samia umekuja siku chache baada ya kuzungumza na Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) na kusema tayari kuna wagonjwa wa Covid-19 nchini kutokana na wimbi la tatu la ugonjwa huo.