Alhamisi , 26th Nov , 2015

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amefuta maadhimisho ya siku ya UKIMWI na kuagiza badala yake, fedha ambazo zingetumika zinunulie dawa za kufubaza makali ya ukimwi ARV.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Omben Sefue imeeleza kuwa Rais ameagiza hilo na taarifa tayari zimekwishasambazwa kwa wahusika ili kulifanyia kazi agizo hilo.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Tume ya kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) Dk.Moris Lekule amesema wamepokea agizo hilo na kwamba kilichofutwa ni sherehe zinazojumuisha kuwaalika viongozi wa kitaifa, vikundi vya ngoma, kusoma hotuba na maadhimisho hayo kufanyika kila mkoa.

Aidha Dk. Lekule amesema badala yake kitakachofanyika siku hiyo ni elimu ya kawaida kuhusu UKIMWI, takwimu na hali halisi ya kitaifa ya ugonjwa huo.