Jumatatu , 13th Apr , 2015

HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE KWENYE SIKUKUU YA KUWEKWA WAKFU NA KUSIMIKWA MHASHAMU ASKOFU LIBERATUS SANGU, KUWA ASKOFU WA JIMBO KATOLIKI SHINYANGA, TAREHE 12 APRILI, 2015

Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo;
Mhashamu Askofu Mkuu, Tarsisius Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania;
Mheshimiwa Balozi wa Vatican, Mhashamu Askofu Mkuu Protase Rugambwa;
Mhashamu Askofu Liberatus Sangu, Askofu Mpya wa Jimbo Katoliki Shinyanga;
Wahashamu Maaskofu Wakuu na Maaskofu;
Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri;
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga;
Viongozi wa Dini na Serikali Mliohudhuria;
Ndugu Waumini,Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana:
Tumsifu Yesu Kristo!

Shukrani na Pongezi
Napenda kuungana na nyote mlionitangulia kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa rehema na baraka zake zilizotuwezesha kushiriki pamoja katika tukio hili muhimu na adhimu kwa Jimbo Katoliki Shinyanga kupata Askofu wake wa nne. Nawashukuru Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania na Jimbo Katoliki Shinyanga kwa heshima kubwa mliyonipa ya kunialika katika sherehe ya kuwekwa wakfu na kusimikwa Mhashamu Baba Askofu Liberatus Sangu kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Shinyanga. Hii ni heshima kubwa kwangu na kwa Serikali yetu na ni kielelezo hai cha uhusiano mzuri uliopo kati ya Kanisa Katoliki na Serikali.
Mhashamu Baba Askofu Liberatus Sangu;

Nakupongeza kwa kuteuliwa kwako na kwa leo hii kukabidhiwa rasmi dhamana ya kuwa Kiongozi Mkuu wa Jimbo Katoliki la Shinyanga. Uteuzi wako kushika wadhifa huu ni uthibitisho wa imani kubwa aliyonayo Baba Mtakatifu Francis kwako. Imani hiyo ndiyo pia waliyonayo wajumbe wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, makasisi, watawa na walei wa Jimbo la Shinyanga. Sote, tumeusubiri uteuzi huu kwa hamu tangu tulipopata pigo la kuondokewa na mpendwa wetu Baba Askofu Aloysius Balina mwaka 2012.
Nakuomba utambue kuwa imani hiyo imebeba matumaini makubwa kwamba utaitenda kazi yako kwa moyo wa dhati, uadilifu na uaminifu mkubwa.

Kwa kawaida matumaini ya waamini kwa kiongozi wao wa kiroho huwa makubwa na wakati mwingine huwafanya wakasahau kuwa kiongozi wa dini pia ni binadamu. Lakini wanafanya hivyo kwa nia njema na kwa sababu nzuri kwamba hakuna mwingine ila wewe. Mimi naamini kwamba kwa malezi mazuri uliyopatiwa na Kanisa lako ukichanganya na uzoevu wako wa muda mrefu wa kazi za kichungaji, uwanazuoni wako na kwa rehema za Mwenyezi Mungu utayamudu vyema majukumu yako ya kuwaongoza kondoo wa Bwana kwenye malisho mazuri ya kiroho na kimwili.

Maadili Mema
Mhashamu Baba Askofu Liberatus Sangu;
Waheshimiwa Maaskofu;
Ndugu Waumini na Wageni Waalikwa;
Malisho ya kiroho huwafanya waumini wawe wacha Mungu. Na, mcha Mungu kwa kawaida humpenda Mungu na jirani yake, huzingatia maadili mema, huwa na tabia njema na mara nyingi huwa raia mwema. Kwa ajili hiyo, viongozi wa dini kama walivyo wa Serikali wanao wajibu maalum wa kulilea taifa. Ninyi mnalea kiroho, kwa maana ya kuwafanya waumini kufuata taratibu za kiimani na sisi tunalea kidunia kwa maana ya raia kufuata taratibu za kikatiba na kisheria na maadili mema kwa mujibu wa mila na desturi za jamii na nchi yetu.

Ninyi viongozi wa dini huwalea waumini kiimani waweze kutende mema hapa duniani ili waje kupata malipo mazuri wanaporejea kwa Muumba wao. Hili la kulea kiimani likifanikiwa basi kwa kiasi kikubwa kazi ya Serikali inakuwa rahisi. Hapatakuwa na watu wanaoiba, wanaoua wenzao, wanaokata albino viungo vyao, wanaotukana wenzao, matapeli, wanaofumaniwa na kadhalika. Hivyo basi, Serikali ingepunguziwa kasi ya kuwakamata, kuwafikisha mahakamani na kuwafunga magerezani watu wengi kama tufanyavyo sasa.

Hivyo basi, mchango wenu katika kujenga maadili mema kwa jamii na watu wake ni kitu kilicho bayana. Aidha, pale tunapokuwa na jamii iliyojaa maovu, umuhimu na ukubwa wa kazi yenu unaonekana bayana. Napenda kutoa ombi maalumu kwako Baba Askofu Sangu pamoja na Maaskofu, Mapadre katika mikoa ya kanda hii kuongeza bidii katika kuelimisha jamii kuacha mauaji ya vikongwe na watu wenye ualbino. Tushirikiane na Serikali kupamba na ushirikina kitu ambacho ndicho chanzo cha mauaji haya na kukatwa viungo albino. Ninyi mnasikilizwa sana, itumieni nafasi hiyo tuondokane na aibu hii.

Mchango wa Kanisa Katika Maendeleo ya Taifa
Waheshimiwa Maaskofu;
Uhusiano kati ya Serikali na madhehebu ya dini likiwemo Kanisa Katoliki ni wa muda mrefu na ni wa kihistoria. Serikali imekuwa ikiunga mkono shughuli za Kanisa katika kutoa huduma za jamii za elimu, afya na nyinginezo zenye kuwaletea maendeleo wananchi. Mmetoa mchango mkubwa sana ambao umewanufaisha Watanzania wengi wa dini na madhehebu mbalimbali. Huduma hizi zimesaidia sana kuongeza kasi ya kuwatoa wananchi kwenye umaskini na kujiletea maendeleo. Tunawapongeza na kuwashukuru sana kwa mchango wenu mkubwa.

Haistaajabishi kuwa matumaini ya waamini wa Kanisa Katoliki, Jimbo la Shinyanga na wananchi wa Shinyanga kwa ujumla juu yako Baba Askofu Sangu siyo ya kiroho pekee. Wanatarajia kuwa chini ya uongozi wako, Kanisa Katoliki litaendelea kutoa huduma za jamii kwao. Wana matumaini hayo kwa sababu wanatambua na kuthamini manufaa makubwa wanayopata katika harakati zao za kujiletea maendeleo kutokana na kazi njema inayofanywa na Kanisa. Wanategemea utaendeleza kazi nzuri zilizofanywa na waliokutangulia na utabuni na kutekeleza miradi mingine mipya ya maendeleo katika Jimbo lako. Nami naungana nao na, sina mashaka juu ya usahihi wa imani yao hiyo kwako.

Ahadi ya Serikali
Mheshimiwa Baba Askofu;
Napenda kukuhakikishia ushirikiano wangu binafsi na ule wa Serikali ninayo iongoza katika kutekeleza majukumu yako ya kiroho na ya huduma za kiuchumi na kijamii kwa maendeleo ya wananchi wa Shinyanga. Pale utakapo ona mchango wa Serikali unahitajika, usisite kuwasiliana nasi. Na iwapo utaona kuna upungufu wo wote sema kwa viongozi wa Wilaya, Mkoa na wa kitaifa: Waziri Mkuu, Makamu wa Rais na hata kwangu. Sisi ni wasikivu. Tuite tutakuitika. Ukituambia tutakujibu kwa lile linalohitaji majibu na tutatenda kwa lile la kufanya, bora tu liwe kwenye uwezo wetu na ni wajibu wetu kufanya.
Wahashamu Maaskofu;

Sisi katika Serikali tunayo kila sababu ya kuendeleza uhusiano mzuri kati yetu na madhehebu ya dini maana kazi muifanyayo haina badala yake. Tunaamini kwa dhati kuwa, kwa pamoja tunaweza kujenga, kuimarisha na kuendeleza amani, umoja na mshikamano uliopo katika taifa letu. Hali kadhalika, tukishirikiana tutaongeza kasi ya kuwawezesha Watanzania kupata maendeleo.
Tutaendelea kutimiza wajibu wetu wa kutengeneza mazingira mazuri kwa madhehebu ya dini kutekeleza majukumu yake. Kuna mambo mawili:

Jambo la kwanza ni kuhakikisha kuwa uhuru wa kuabudu unakuwapo nchini, unaheshimiwa na unatekelezwa kwa vitendo. Hii ni haki inayotambulika na Katiba yetu ya sasa na utekelezaji wake hauna kasoro. Bahati nzuri imesisitizwa na kufafanuliwa vizuri zaidi katika Katiba Inayopendekezwa.

Pili, tutaendelea kushirikiana na kusaidiana kwa upande wa shughuli zenu za huduma za kiuchumi na kijamii mzifanyazo. Tumekuwa tunatoa misamaha ya kodi kwa shughuli za madhehebu ya dini na hata kuchangia fedha za Serikali na watumishi kwa baadhi ya shughuli zenu hasa za afya na mikopo ya wanafunzi katika vyuo vikuu.

Tutaendelea kufanya hivyo kwa kutambua mchango muhimu unaotolewa na huduma hizo kwa maendeleo ya nchi yetu na ustawi wa watu wake. Maombi yangu au yetu kwenu ni kuwa msiwaruhusu watu waovu wakaitumia vibaya fursa hii muhimu. Tunapopata taarifa za fursa hiyo kutumika kinyume hutusumbua sana.

Tuendako
Mwadhama Kardinali;
Waheshimiwa Maaskofu;
Wageni Waalikwa;
Wakati wote sisi viongozi wa Serikali na dini tunao wajibu wa kipekee katika uhai wa taifa letu na watu wake. Tunalo jukumu maalum la ulezi, yaani kuhakikisha watu katika nchi yetu wanaishi kwa amani, umoja, upendo na mshikamano licha ya tofauti zetu za rangi, kabila, dini, jinsia, maeneo tutokako, au ufuasi wa vyama vya siasa. Naomba tukumbuke kuwa tofauti hizi ambazo hatuna budi kuishi nazo, tusiziache zikawa nyufa za uhasama ambao siyo tu zitaligawa taifa bali zinaweza kulimong’onyoa na kulisambaratisha.

Sisi viongozi tuna wajibu wa kihistoria wa kutambua kuwa ni jukumu letu kuhakikisha kuwa hilo haliwi. Nayasema haya kwa sababu. Kwa jumla tunapita katika kipindi kisichokuwa cha kawaida, ambacho kama hatutafanikiwa kubadili mwelekeo huu kunaweza kuwepo madhara makubwa. Nawaahidi ushirikiano wangu binafsi na wa Serikali ninayoiongoza. Naomba viongozi wa dini msaidie ufa usiwe mpana zaidi.

Tumieni Kamati za dini kwa mwaka kama huu wa uchaguzi ambapo baadhi ya wanasiasa na washabiki wao katika tamaa yao ya kupata madaraka hupenda kuzitumia tofauti hizi kwa maslahi yao binafsi na vyama vyao, tunaomba muwe makini zaidi. Wakati mwingine wanasiasa hufanya makusudi kuchochea uhasama kwa kutumia tofauti zetu za asili ili wapate manufaa ya kisiasa. Wao hawajali inayoweza kutokea na madhara makubwa kwa nchi yetu.

Kwa ajili hiyo, niwaombe viongozi wa dini tutumie vizuri nafasi ya uongozi mliyojaaliwa na Mwenyezi Mungu kuzuia wanasiasa wasilifikishe taifa pabaya. Watakeni waumini wenu wasiwasikilize na kufanya mambo yote yanayofarakanisha jamii bali washikilie yale yanayowaunganisha na kuleta utangamano. Na lililo muhimu kuliko yote ninalowaomba msiwape wanasiasa fursa kuingiza dini kwenye siasa au siasa kwenye dini.

Tuambieni bila kigugumizi. Wasiziache dini ziwe huru kwa watu wa vyama vyote. Makanisa na Misikiti ibaki kuwa nyumba za ibada na siyo majukwaa ya siasa. Iwe mahali pa kuwaunganisha wote na viongozi wa dini wawe kimbilio lao wakati wanapogombana.

Msikubali ufuasi wa vyama vya siasa ukawafarakanisha viongozi wa dini mpaka mkapoteza dira na nafasi yenu muhimu ya uongozi wa waamini wenu. Kuchanganya dini na siasa ni hatari sana kwa usalama, amani na utulivu wa jamii na hata dini zenyewe. Si vyema wakati wa Chama cha siasa kushindwa kukawa ni kushindwa dini fulani na waumini wake au Chama na kushinda ni kwa dini nyingine na waumini wao.

Wafuasi wa vyama vya siasa kugombana si jambo la ajabu. Je itakuwaje kama dini zimehusishwa na kugawanyika kidini. Ugomvi huo unakuwa na sura ya ugomvi baina ya wafuasi wa dini tofauti kwa mwamvuli wa siasa? Kuna hatari ya kuzuka vita vya kidini na nchi ikawaka moto. Kunaweza kutokea maafa yasiyotabirika sura yake na mwisho wake. Naomba viongozi wa dini mtambue wajibu wenu wa kuponya.

Tuwaache waumini wawe wafuasi wa vyama vya siasa wavipendavyo. Kwa uchaguzi muwahimize waumini wenu wachague kwa busara kadri watakavyoridhishwa na sera, ilani na ahadi za vyama vya siasa na wagombea wao. Wasisitizeni kujali ubora, moyo wa uzalendo na uadilifu wa wagombea. Tukifanya hivyo tutavuka salama. Kinyume chake inaweza kuzua tatizo.

Hitimisho
Mheshimiwa Baba Askofu;
Leo ni siku ya furaha kwetu sote. Ni siku pia ya kumsifu Mwenyezi Mungu kwa neema zake na kumshukuru kwa uteuzi wako. Waumini waliofurika hapa wamekuja kwa ajili ya sherehe za kuwekwa wakfu na siyo Mkutano wa Rais. Niruhusu niishie hapa nitoe nafasi kwa kuabudu na kumtukuza Mungu wetu. Nitatafuta wasaa mwingine mwafaka wa kuzungumza na wananchi wa Shinyanga na Watanzania kwa jumla kuhusu mambo ya maendeleo.

Nikushukuru tena kwa kunialika na kwa kunipa heshima hii ya kuzungumza na viongozi wa Kanisa, waumini na wananchi. Mwenyezi Mungu na akubariki Baba Askofu na akufanyie wepesi katika majukumu yako.
Asanteni kwa kunisikiliza.