Alhamisi , 2nd Jun , 2016

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli amesema atasaidia kupatikanna kwa bilioni 10 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa mabweni ya wanafunzi Chuo Kikuu cha Dar es salaam ili kusaidia wanafunzi wengi wanaolazimika kupanga nje ya chuo.

Rais Magufuli ameyasema hayo leo wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa maktaba ya kisasa Chuo Kikuu cha Dar es salaam.

‘’Uzuri mimi nafahamu ukandarasi vizuri nikitoa advance bilioni 10 ujenzi wa mabweni utaanza mara moja tafuteni mkandarasi kazi hiyo ianze katika ardhi ya chuo hiki mimi nitasaidia upatikanaji wa fedha ili tusaidie wanafunzi wengi wanaopata tabu kwa kukosa mabweni”-Amesema Rais Magufuli.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Kikwete amesema kwamba Chuo kinakabiliwa na uchakavu wa miondombinu ikiwa ni pamoja na upungufu mkubwa wa mabweni ambapo wanafunzi wanaolala ndani ya chuo ni 30% huku 70% wakiwa hawajulikani wanakolala.