Alhamisi , 7th Sep , 2023

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, amesema usimamizi makini wa serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amewezesha Taifa kuvuka malengo ya kupambana na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI (VVU)ya 95-95-95 yaliyopangwa kufikiwa mwaka 2025.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa

Ameyasema hayo leo Septemba 7, 2023, katika kilele cha mdahalo wa kitaifa juu ya kuimarisha ubia baina ya serikali, wadau na jamii kwa uendelevu wa mafanikio ya  mwitikio wa UKIMWI nchini uliofanyika jijini Dodoma.

"Leo hii tayari asilimia 96 ya watu wanaoishi na mambukizi ya VVU wanajua hali zao, asilimia 98 ya wanaojua hali zao wapo kwenye tiba ya ARV na kati yao, asilimia 97 wameweza kufubaza wingi wa virusi kwenye damu, jukumu kubwa la Taifa tulilonalo ni kulinda na kuyaendeleza mafanikio haya  kwa nguvu za pamoja na umoja hadi tufikie malengo ya sifuri tatu ifikapo mwaka 2030," amesema Waziri Mkuu

Waziri Mkuu amesema serikali itaendelea kuimarisha uwekezaji na mifumo endelevu ya upatikanaji rasilimali fedha kwa ajili ya afua mbalimbali za UKIMWI ikiwa ni pamoja na Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti UKIMWI (AIDS Trust Fund) na mipango mbalimbali katika ngazi ya Halmashauri na Taifa kwa ujumla ili malengo ya kutokomeza ugonjwa huo yaweze kufikiwa.

Akizungumzia kuhusu majumuisho yaliyotokana na mdahalo huo, Waziri Mkuu amewahakikishia  wadau na Watanzania wote kuwa Serikali imesikia na kupokea yote yaliyotajwa katika mdahalo huo kutoka kwa Mwenyekiti wa Baraza la Watu Wanaoishi na VVU (NACOPHA) na itayafanyia kazi. “Suala la ubia halikwepeki tunatambua umuhimu wa ushirikiano na tutalitekeleza kwa maslahi mapana ya Watanzania"