Awali kabla ya kufikishwa katika mahakama hiyo Profesa Lipumba alifika katika kituo cha polisi ambapo alitakiwa kuripoti yeye na viongozi wengine wa chama hicho ambao walikamatwa katika tukio la maandamano na baada ya kiongozi huyo kuzungumza na polisi aliruhusiwa kuondoka na ndipo alipozungumza na waandishi wa habari kulaani kilichofanywa na polisi.
Akisimulia namna alivyopata kipigo hadi kupasuka sehemu ya kichwani Naibu Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa chama hicho Bw Abdul Kambaya amesema anakumbuka silaha mbalimbali zilitumika ikiwemo spana ya kufungua tairi ya gari ambayo ndiyo iliyomjeruhi kichwani.
Wakati viongozi hao wa CUF wakiendelea kufanya mahojiani mbalimbali na waandishi wa habari alikuja afisa mmoja wa polisi na kumwita profesa Lipumba na kuondoka naye kuelekea katika moja ya ofisi zilizopo kituoni hapo.
Baada ya muda wa takribani saa moja na nusu hali ya kiongozi huyo ilibadilika na kukimbizwa katika kituo cha afya cha umoja wa mataifa kilichopo karibu na viwanja vya Leaders akiwa chini ya ulinzi mkali wa jeshi polisi katika gari lenye namba za usajili PT 2566 aina ya RAV 4.
Baada ya matibabu msafara wa polisi ulielekea katika mahakama ya kisutu ambapo wakili wa serikali Joseph Maugo mbele ya hakimu mkazi Mh Isaya Khalfani aliiambia mahakama kuwa kati ya tarehe 22 na 27 January mwaka huu akiwa kama kiongozi wa chama, aliwashawishi wafuasi wake kutenda kosa la jinai na kuongeza kuwa upelelezi haujakamilika na hawana pingamizi na dhamana.
Upande wa wanasheria wanaomtetea Prof. Lipumba, wapo sita wakiongozwa na wakili Mohamedi Tibanyendela na Peter Kibatala ambapo waliomba mahakama itoe masharti mepesi.
Prof Lipumba yupo nje kwa dhamana ya watu wawili waliosaini bondi ya shilingi milioni mbili na shauri hilo litatajwa tena Feb 26 mwaka huu.