Jumatano , 3rd Apr , 2019

Jeshi la Polisi Tanzania limeendesha Operesheni sehemu mbalimbali za nchi ili kupambana na wahalifu waliokuwa wanavamia majumbani na kuteka magari njiani kwa kutumia silaha za moto.

Kamishna Liberatus Sabas akiwa ameshika silaha

Kamishna wa Operesheni na Mafunzo ya Jeshi la Polisi Nchini CP, Liberatus Sabas amesema operesheni hiyo iliyofanika katika Mkoa wa Kigoma, imefanyika ndani ya miezi mitatu kuanzia Januari mpaka mwezi Machi mwaka huu na kufanikiwa kukamata silaha 14 aina ya SMG na risasi 350.

Pamoja na mafanikio hayo, Jeshi la Polisi limefanikiwa kuua majambazi 24 katika majibizano ya kurushiana risasi na polisi ambapo katika mapambano hayo askari wawili walijeruhiwa na majambazi ila mpaka sasa wanaendelea na matibabu.

Aidha kamishna Sabas, amesema wahalifu hao wanatoka nchi za jirani ambazo hazina utulivu wa kisiasa, huku akiwaonya wahalifu hao wanaotoka nchini jirani kuwa wajue wataingia ila hawatatoka na wakae wakijua hakuna mwalifu atakaebaki salama.

Pia akiwataka wale wanaoingia nchini kwa kutumia miamvuli ya wakimbizi na wao hawatakuwa salama kwani Tanzania ni kisiwa cha amani.

Kamishna Sabas amewataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano baina yao na Jeshi la Polisi ili kukabiliana na wahalifu wa ndani na wale wanaotoka nje ya nchi na kuwatumia salamu kuwa Tanzania si sehemu salama kwa wahalifu.

Bonyeza hapa chini, Kamishna Sabas akielezea.