Jumanne , 3rd Nov , 2015

Jeshi la polisi kanda maalumu ya Dar es Salaam limepiga marufuku maandamano yasiyo na kikomo yalipangwa kufanywa leo na Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA kwa madai ya kuporwa ushindi wa kiti cha Urais kwa Mgombea wao Edward Lowassa.

Kamishna wa polisi wa Kanda Maalum ya Dar Es Salaam Suleiman Kova

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam kamishana wa jeshi la polisi kanda maalimu ya Dar es Salaam Kamishna Suleiman Kova amesema kuwa kuitishwa kwa maandamani hayo hakujafuata sheria hivyo jeshi la polisi haliwezi kuyasimamia.

Aidha Kamanda Kova amesema pia jeshi haliwezi kulinda maandamano yasiyokuwa na kikomo wala kujulikana yaanzia wapi na kuishia wapi huku akitoa onyo kwa watakaojitokeza katika maandamano hayo sheria itachukua mkondo wake.

Kamanda Kova ameongeza kuwa utaratibu wa jeshi ni barua iweze kupelekwa masaa 48 kabla ya maandano kuitishwa na kusema barua hiyo imechelewa kufika hivyo polisi wanasheria ya kuyazuia maandamano hayo.

Aidha amesema kuwa kama kuna chama hakijaridhika na ushindi uliopatika katika uchaguzi mkuu kuna sheria za kufuata ikiwemo mahakama na vyombo vingine lakini si kuwashinikiza wananchi waandamane.

Ameongeza kuwa kufanyaka kwa maandamano hayo kutawakosesha fursa wananchi wengine ambao riziki yao wanaipata kwa siku na kusimamisha shughuli za kujenga uchumi kwa muda usiojulikana jambo halikubaliki nchini Tanzania.