Jumanne , 5th Mei , 2015

Kamanda wa polisi mkoani Arusha, Liberatus Sabasi alilazimika kukaa kwa masaa zaidi ya mawili, standi kubwa ya mabasi na kuwalazimisha wenye mabasi makubwa waliogoma, kuyaondoa magari hayo kwa haraka kabla ya kuyavuta kituo cha Polisi.

Kamanda wa polisi Mkoani Arusha, Liberatus Sabasi.

Wakati Kamanda akiwaamuru wenye mabasi makubwa hali ilikuwa tofauti kwa madereva wa daladala, wao wamegoma kwa staili tofauti, hawaonekani kabisa barabarani na baadhi ya magari kuonekana yamepakiwa kwenye vituo vya mafuta, huku abiria wakitumia usafiri wa bajaji, kilikuu na pikipiki.

Akizungumza kwa hasira katika stendi ya magari hayo, Sabasi amesema kama walifahamu kuna mgomo wasingeyaleta kituo cha mabasi wangepaki majumbani mwao, ila kwa sababu wameyaleta na kuchukua fedha za abiri lazima wayaondoe.

Sabasi amewatahakikishia wenye magari hayo kuwa barabara ipo salama na hakuna atakayewapiga njiani na yeye ndiyo mwenye kulinda usalama wao hivyo wasiogope.

Hata hivyo pamoja na kuwasihi madareva hao kuondoka hawakutaka kuondoka mpaka pale askari wa usalama barabarani, walipoamua kutoa namba za usajili ya baadhi ya mabasi ili wayafuate kituoni, ndipo walipoamua kuyaondoa mabasi hayo majira ya saa 4:43 asubuhi.

Magari ambayo yalionekana kuondoka kituoni hapo muda huo ni pamoja na lenye namba T. 128 CZB la kampuni ya Osaka Classic, T.726 CUU kampuni ya Safari Luxury na T. 265 ALR la kampuni ya KVC Safari, huku mabasi ya kampuni ya Sai Baba zaidi ya manne yakiondolewa bila abiria na kudai wameamriwa na tajiri wao yaende kwenye eneo lao kupaki hadi hali itakapokuwa shwari.

Mmoja wa madereva hao, Gidion Ngomuo, alisema kuwa kitu kikubwa wanachogomea madereva wana madai mengi kama vile kulipwa posho ya Sh. 13,000 kwa siku huku wakilala nyumba za wageni na kula, fedha ambayo ni ndogo.

Pia amesema mishahara midogo ambapo wanalipwa Sh. 200,000 kiwango ambacho hakitoshi na wamegoma ili kushinikiza serikali ikae chini kati yao, madereva na polisi wa usalama barabarani waweke mambo sawa.

Ngomuo amesema kikubwa siyo kulazimishwa kuyatoa magari bali wakubaliane, kinyume na hapo ajali zitaendelea kutokea sababu madereva wanafanya kazi mazingira magumu na mawazo wanayo mengi kuhusu maisha, kutokana na kipato kidogo.