![](http://eatv.tv/sites/default/files/styles/detailpageimg/public/news/2024/04/27/Untitled-2.jpg?itok=EQGDOtB6×tamp=1714203238)
Polisi wamesema miongoni mwa taarifa za uzushi zinazosambaa mitandaoni ni zile zenye kichwa cha habari SHUHUDA ambazo zinaeleza kuwa "Zuchy kapata ajali na boda hit and run mbele ya mataa ya masana kama 100 mita hivi toka saa nane usiku dereva wa boda akapelekwa hospital. Umoja wa bodaboda wamekaa na mwili barabarani pale wakiita Polisi kisingizio gari haina mafuta kweli. Pia taarifa hiyo inaeleza bodaboda walikaa na mwili hadi wakafunga barabara ili kushinikiza Polisi waitwe."
Polisi wamesema usahihi wa tukio hilo ni kuwa tukio hilo liliripotiwa saa kumi na dakika kumi na mbili alfajiri kuwa, kuna ajali imetokea eneo la Mbezi Makonde. Baada ya kupokelewa taarifa hiyo Maafisa na Askari waliokuwa kwenye majukumu katika mkesha wa Tamasha la Shangwe la Utawala lililokuwa linafanyika eneo la Tanganyika Packers waliondoka wakiwa na gari ya Polisi kuelekea eneo la tukio na kuchukuwa mwili wa marehemu na kuupeleka Hospitali ya Mwananyamala kwa taratibu zingine za kisheria.
Taarifa ya Polisi inaeleza kuwa katika uchunguzi imebainika marehemu alipata ajali na pikipiki aliyokuwa amepanda yenye namba MC 436 CMU iliyokuwa ikiendeshwa na dereva ambaye alipata majeraha na anaendelea na matibabu.
Hivyo, mara baada ya taarifa ya tukio hilo kutolewa na kupokelewa, Maafisa na Askari Polisi walifika kwenye tukio kwa wakati na kutekeleza yale yanayopaswa kutekelezwa kwenye eneo la ajali. Tunawashukuru bodaboda wa eneo hilo wanaojali utu wa binadamu kwa kuzuia magari yasimkanyage marehemu.