Jumanne , 12th Oct , 2021

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za mauaji ya Mtendaji wa mtaa wa Mbezi Msumi, aliyejulikana kwa jina la Kelvin Costa Mowo (38), wakati akitekeleza majukumu yake ya kusikiliza wananchi ambao walikuwa na mgogoro wa ardhi.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Muliro Jumanne

Akizungumzia tukio hilo Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo Muliro Jumanne, amesema tukio hilo limetokea jana Oktoba 11, majira ya saa 5:54 asubuhi huko eneo la Msumi Mbezi wilaya ya Ubungo katika ofisi za serikali ya Mtaa.

Amesema kuwa ghafla watu wapatao wanne waliingia ofisini na mmoja wao akatoa panga na kumshambulia mtendaji huyo kitendo kilichopelekea kupata majeraha makubwa na baadae akapoteza maisha wakati akikimbizwa hospitalini.