Jumanne , 23rd Mei , 2023

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, limesema kwamba Joel Misesemo aliyejirusha ghorofani kwenye jengo la Derm Plaza Makumbusho na kufariki dunia hii leo Mei 23, 2023, amejirusha kwa makusudi kupitia dirisha lililopo ghorofa ya saba.

Kushoto ni Joel Misesemo aliyefariki kwa kujitupa ghorofani na kulia ni Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam SACP Jumanne Muliro

Taarifa hiyo imetolewa na Kamanda wa Kanda hiyo SACP Lazaro Mambosasa, amesema mifumo ya kamera ya jengo hilo imeonesha marehemu alivyojirusha, na kwamba gari lake limehifadhiwa na uchunguzi wa kina wa tukio hilo unaendelea.

"Uchunguzi wa awali unaonesha kuwa marehemu alionekana katika jengo hilo tarehe 23, Mei 2023 majira ya saa 11:40 alifajiri na alimwambia mlinzi wa zamu kuwa anaenda kufanya ibada kwenye msikiti uliopo ghorofa ya 15 ndani ya jengo hilo, hata hivyo muda mfupi baadaye alijirusha kutoka juu ghorofani na kuanguka chini," imeeleza taarifa ya SACP Muliro

Tarifa hiyo imeendelea kueleza, "Aidha mifumo ya kamera ya jengo hilo inamuonesha mtu huyo akijirusha kwa makusudi kutoka ghorofa ya saba kupitia dirishani, mwili wake umepelekwa Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala kwa uchunguzi zaidi,"

Aidha Jeshi la Polisi limepata gari la marehemu aina ya Suzuki rangi ya silver lenye namba za usajili T142 DRM lililokuwa limeegeshwa kwenye maegesho ya magari katika eneo hilo na limehifadhiwa kituo cha Polisi Oysterbay, na kwamba uchunguzi wa kina unaendelea juu ya tukio hilo.

Imebainika kwamba Joel Misesemo pia alikuwa akijishughulisha na shughuli za ushereheshaji (MC).