Jumatatu , 6th Jan , 2020

Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro, linawashikilia watu 14 kwa makosa mbalimbali ikiwemo kukamatwa na vipande vya pembe za ndovu 13 vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni mia moja thelasini na saba (137,576,250), pamoja na kukutwa na Gobole 4 zilizotengenezwa kienyeji. 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, SACP Wilbroad Mutafungwa.

Akizungumza na Waandishi wa Habari, Kamanda wa Polisi mkoani humo, SACP Wilbroad Mutafungwa, amesema kuwa katika oparesheni zilizofanyika mwishoni mwa mwaka 2019 kwa Jeshi hilo kwa kushirikiana na Mamlaka ya Wanyamapori nchini (TAWA), jumla ya vipande 13 vimekamatwa katika pori la akiba la Serou.

Katika tukio jingine Jeshi hilo linawashikilia watu 7, wanaojihusisha na mtandao wa wizi wa Ng’ombe 80 na kondoo 52, sambamba na kukamata magari mawili aina ya Toyota Noah yenye namba za usaji T 309 CYS na Toyota Hiace yenye namba za usajili T 914 DFY, ambazo zilikuwa zikitumika kusafirishia nyama za wizi.

Kamanda Mutafungwa ameyataja majina ya watu waliokamatwa katika matukio hayo kuwa ni Abdallah Mputa, Fikiri Salum, Daniel Mbena, Salum Ally na Novatus Kabinda wote wakazi wa Ulanga, huku wengine wawili waliokutwa na pembe 2 za ndovu, wakiendelea kutafutwa baada ya kufanikiwa kutoroka.