Jumanne , 16th Feb , 2016

Naibu waziri wa mambo ya ndani Yusuph Masauni amelitaka jeshi la polisi Kisiwani Zanzibar kuhakikisha amani na usalama vinakuwepo kabla na baada ya uchaguzi wa marudio kisiwani humo.

Masauni ameyasema hayo wakati akizungumza na jeshi la polisi kisiwani Pemba ambapo amewataka kujiimarisha katika kupambana na uhalifu wa aina yoyote utakaojitokeza katika kuelekea uchaguzi wa tarehe 20 mwezi Machi 2016.

Naibu waziri huyo pia amelitaka jeshi la polisi kuharakisha ripoti ya hali ilivyokuwa kwa uchaguzi ulioahirishwa na kusababisha kutangazwa kwa marudio ya uchaguzi ili kuweza kujifunza kuepuka kasoro ambazo zilijitokeza.

Aidha akijibu swali kuhusu nyumba za watu kuwekwa alama ya X, kuchomwa moto kwa mashamba ya karafuu na kuchomwa ofisi ya CCM Kingeja, Kamishna wa polisi Zanzibar Hamdani Omary Makame amesema jeshi hilo linawashikilia watu 7 kwa kuhusishwa na matukio hayo na jeshi hilo lipo imara kuhakikisha usalama wa raia na mali zao upo kisiwani humo.